Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalum ya Uwekezaji
nchini (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru
akimkabidhi leseni ya uwekezaji Mkurugenzi wa Mambo Coffee Co. Ltd, Bw.
Athanasio Massenha mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Mamlaka hiyo ilikabidhi leseni hizo kwa
wawekezaji wapya sita.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalum ya Uwekezaji nchini (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru akimkabidhi leseni ya uwekezaji mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Sheikh Motors Ltd mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Mamlaka hiyo ilikabidhi leseni hizo kwa wawekezaji wapya sita.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA)
imekabidhi leseni za uwekezaji katika maeneo yake kwa makampuni mapya sita.
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru alikabidhi leseni
hizo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na kusema kuwa hatua hiyo ni
ithibitisho wa nia ya mamlaka yake kuendeleza sekta ya viwanda hapa nchini.
“Kuendeleza sekta ya viwanda ni moja ya ajenda kuu ya mamlaka
yetu,” aliwaambia waandishi wa habari baada ya kukabidhi leseni hizo.
Kampuni zilizokabidhiwa leseni ya EPZ ni pamoja na Kokoa
Kamili Ltd, Rift Valley Tea Ltd, Mambo Coffee Ltd, Sheikh Motors Ltd, Afriweld
Industries Ltd na Tanzania Macenta Co Ltd.
Kampuni hizo zimejikita katika kuendesha viwanda vya kuongeza
thamani mazao na vitu mbalimbali hapa nchini.
Kati ya kampuni hizo sita; mbili ni za wawekezaji toka
Uingereza na Marekani wakati mbili nyingine ni za ubia kati ya watanzania na
wawekezaji wenzao toka nchi za Ukraine na India. Kampuni mbili zilizobaki zinamilikiwa kwa
asilimia mia moja na wawekezaji wazawa.
Jumla ya uwekezaji wa uliofanywa na kampuni hizo ni dola za
Marekani milioni 17 na zinatarajiwa kuzalisha ajira mpya zaidi ya 700. Pia, thamani ya mauzo ya nje ya kampuni hizo
kwa mwaka yanatarajiwa kufikia zaidi ya dola za kimarekani milioni 23 kwa
mwaka.
Dkt. Meru alisisitiza kuwa nchi zote zilizopata maendeleo
zilifanya jitihada kuwekeza katika viwanda na kwamba ni muhimu pia Tanzania
ifuate mkondo huo.
“Hatuwezi kupata maendeleo ya maana kama hatutawekeza kwenye
viwanda…na hiki ndicho tunachojaribu kufanya,” alisema Dkt. Meru.
Alisema viwanda vitazalisha ajira, kuleta fedha zaidi,
teknolojia na kuongeza thamani mazao kwa malighafi za hapa nchini.
Alisema kwa sasa, Tanzania inapata hasara kwa kiwango cha juu
kutokana na kuuza mali ghafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani na kwamba
hali hii inatakiwa kurekebishwa haraka.
“Unapouza mali ghafi nje unageuka kuwa soko la bidhaa hizo
hizo baada ya kuongezwa thamani,” alisema, na kueleza kwamba ujio wa kampuni
hizo unalenga kupunguza tatizo hilo.
Dkt. Meru aliwaambia viongozi wa kampuni hizo kuwa kwa
kufanya kazi katika maeneo ya mamlaka hiyo, watafaidika na kuona umuhimu wa
kufanya kazi na EPZA.
“Sisi pia ni kama daraja kwa taasisi nyingine za serikali,”
alisema na kuongeza kuwa mamlaka yake itaendelea kuwasaidia na kuhakikisha kuwa
wanapata mafanikio.
Alisema baadhi ya makampuni yatafanya kazi katika mikoa
mingine nje ya Dar es Salaam na kueleza kuwa hii ni hatua njema inayoonyesha
kuwa sasa Tanzania inaanza kufunguka.
Kuhusu kampuni zinazomilikiwa na watanzania alisema huo ni
uthibitisho kuwa watanzania wanaweza na kuwa wengine waige mfano huo kwa faida
yao nay a nchi.
Mkurugezi wa Mambo Coffee Co. Ltd, Bw. Athanasio Massenha
alisema walihamasika kuomba leseni ya EPZ baada ya kugundua vivutio vya
uwekezaji vinavyotolewa na mamlaka hiyo kwa wawekezaji.
“Kama wawekezaji wazalendo, tunafurahia hatua hii muhimu,”
alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Utawala na Masoko wa Rift Valley
Tea Solutions Ltd, Bw. Dilip Rughani alisema leseni hiyo na kwamba itawawezesha
kuwa washindani wazuri katika eneo hili la Afrika.
“Hii itatuwezesha kushindana na kampuni kama yetu zilizo nchi
jirani,” alisema na kuongeza kuwa itawasaidia kupanua biashara yao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment