Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi ya Wahandisi wa Umeme na Elektroniki
Duniani (IEEE) imeishauri sekta ya viwanda na kampuni mbalimbali nchini
kusaidia kufanya tafiti ili kuja na ubunifu ambao utasaidia maendeleo na kukuza
ustawi wa jamii.
Rais wa Taasisi hiyo tawi la
Tanzania, Dkt. Zaipuna Yonah ambaye pia ni Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia cha Nelson Mandela aliwambia waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki kuwa sekta binafsi ina wajibu wa kufanya tafiti kusaidia
jamii.
Alikuwa akizungumza wakati wa ziara
ya Rais Mteule wa taasisi hiyo kubwa dunaini, Dr. Roberto de Marca aliyekuwa
nchini kukutana na wanachama na kuhamasisha sayansi na teknolojia.
“Taasisi yetu inapenda kuona sekta ya
viwanda na kampuni zinazidisha juhudi katika eneo hili muhimu na siyo kuiachia serikali peke yake kufanya tafiti
hizo,” alisema.
Alisema hadi sasa viwanda na
makampuni nchini vinaangalia zaidi kufanya biashara na kutengeneza fedha,
wakati wanaweza kuingia katika eneo hilo la tafiti na kuja na huduma mpya na
kutengeneza fedha zaidi.
Akitoa mfano alisema huduma ya Mpesa
ni ubunifu uliofanywa hapa nchini na watanzania na inatumiwa na watu wa vipato
vyote, na kwamba ubunifu wa namna hii ukiendelea utazidi kuboresha huduma na
maendeleo ya taifa.
“Taasisi hii inatambua taaluma 11 za sayansi zikiwemo uhandisi
wa aina zote na wataalamu wote
wanaotumia TEHAMA wanaruhusiwa kujiunga,” alisema.
Naye Rais wa taasisi hiyo, Profesa
Roberto B.de Marca alisema Tanzania inatakiwa kuwekeza zaidi katika elimu na
kutoa motisha kwa wanafunzi katika masomo ya sayansi.
“Natambua nchi hii ina vyuo vikuu vya
kutosha na vinaweza kuzalisha wahandisi wengi na bora,” alisema na kuongeza
kuwa kinachohitajika ni kuwekeza zaidi eneo hili.
Aliongeza kusema kuwa wahandisi
wakiwa wengi na bora husaidia kukuza uchumi na kuanzisha miradi ambayo itatoa ajira
kwa jamii.
Alisema dhamira ya taasisi yake ni kuona
Afrika na Tanzania ikiwa mojawapo inaongeza wahandisi ili kuwa chachu ya maendeleo.
Alisisitiza kuwa taasisi yake
itaendelea kuwa karibu na wanachama wake wa Tanzania na kuwahamasisha wahandisi
kufanya tatifi ili kusaidia nchi.
Mwanafunzi anayesomea Uhandisi (BSC Computer Engineering & IT) Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Bi. Tumwagile Gedion alisema TEHAMA ina nafasi kubwa
ya kubadilisha maisha ya binadamu.
“Tumekutana na Rais wa taasisi hii na
tumejifunza vitu vingi...mimi na wenzangu tunajiunga nayo ili kuwa wanafamilia
wa taasisi hii muhimu duniani,” alisema.
Alisema Tanzania inaweza kuendelea
kama itaweka vipaumbele vya kuendeleza taaluma hiyo ikiwemo kukuza miundombinu
ya elimu ili wanafunzi wapende kusoma masomo ya sayansi.
Akiwa chini pamoja mambo mengine, Rais
huyo alikutana na wanachama wa taasisi hiyo na wanafunzi wa fani za uhandisi wa
vyuo vikuu mbalimbali, kikiwemo Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), na ST.
Joseph Engineering.
Taasisi hiyo yenye makao makuu nchini
Marekani ina wanachama 425,000 duniani katika nchi 160. Kuna jumla ya wanachama
100 Tanzania.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment