Wednesday, November 6, 2013

EPZA yahamasisha uwekezaji katika viwanda vya Korosho

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) imehamasisha uwekezaji katika viwanda vya kubangua na kusindika korosho na kusema kwamba iko tayari kupokea wanaotaka kufanya hivyo na kuwasaidia katika maeneo yake ya uwekezaji.
Imesema Tanzania bado haina viwanda vya kutosha vya kubangua korosho hali mabayo inarudisha nyuma sekta ndogo ya uzalishaji zao hilo.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji na Huduma wa Mamlaka hiyo, Bi. Zawadia Nanyaro aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wa sekta hiyo ndogo ya kilimo hivi karibuni jijini Dar es Salaam kuwa viwanda vya kubangua korosho bado havitoshi na hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya uzalishaji zao hilo muhimu.
“Zao hili ni moja kati ya mazao muhimu yakiwemo ya kahawa, tumbaku, pamba na Korosho yenyewe ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi...lakini linakabiliwa na tatizo la uchache wa viwanda,” alisema.
Alisema mamlaka yake inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia programu za mamlaka hiyo kuwekeza katika viwanda vya kubangua korosho ili kuondoa tatizo hilo na kukuza uzalishaji.
Alifafanua kuwa wawekezaji wa nje wanapofika kuwekeza wanasaidia wawekezaji wa ndani kupata maarifa, ujuzi na teknolojia na hiyo ndiyo njia ya kuleta maendeleo.
“Tunashukuru mkutano huu wa wadau kufanyika kwa vile tumeweza kutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa washiriki kutumia fursa za uwekezaji ndani ya programu za mamlaka,”alisema Bi. Zawadia.
Aliongeza kusema kuwa njia ya kuondokana na hali duni ya uzalishaji na vipato ni kutumia fursa zilizopo ili kujikwamua kwa faida ya taifa zima. 
Alisema zaidi ya asilimia 90 ya korosho inayozalishwa hapa nchini huuzwa bila ya kuongezewa thamani na kusababisha wakulima kushindwa kupata faida stahiki.
“Nchi haitaweza kupiga hatua na wakulima watabaki kuwa masikini kama nchi itaendelea kuuza korosho bila ya kuongezewa thamani,” alisema na kuongeza kuwa EPZA inalenga kuondokana na tatizo hilo.
Alisema mamlaka hiyo inahamasisha uzalishaji na uongezaji thamani mazao ili kujiepusha na uuzaji mazao yakiwa ghafi katika masoko ya nje.
Kwa Upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Mungano  Vyama vya Wakulima wa Korosho Afrika (Africa Cashew Nuts Alliance), Bw. Maokola Majogo alisema kuna kila sababu ya serikali kushirikiana na wadau wa korosho kupata masoko ya uhakika
“Zao hili ni muhimu sana kwa mikoa ya kusini katika kujipatia vipato...ni lazima lipewe kipaumbele na masoko yake yawe ya uhakika,”alisema.
Alisema anamuomba waziri wa Viwanda na Biashara kutembelea viwanda vya kusindika ili kujua matatizo yanayowasibu na kuchukua hatua ya namna ya kuondokana na matatizo hayo.
Aidha alisema sekta hiyo inakabiliwa na tatizo la mikopo kuwa na riba kubwa na kusababisha shughuli za uzalishaji korosho katika mnyororo wake kushindwa kufikia malengo yake.
Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Chakula na Masoko, Bw. Christopher Chiza, mikoa hiyo ya kusini ina uwezo wa kuzalisha tani 154,000 za korosho na mipango ya serikali ni kuona inafikia tani 300,000 kwa mwaka.
“Sasa hivi tunazungumza tufike sehemu mazao ya kahawa, tumbaku, pamba na korosho yanapopata matatizo ya masoko ya nje basi yaweze kupatiwa ruzuku kuzuia kuporomoka kwa uzalishaji,” alisema.
Alisema mikakati ya namna hiyo itawezesha uzalishaji kutotetereka ili nchi iweze kupiga hatua kwa sababu mazao hayo ni muhimu kwa uchumi.
Mkutano wa wadau wa sekta hiyo ndogo ya Kilimo ulifanyika jijini Dar es Salaam ukishirikisha wadau mbalimbali kupata fursa ya kujadili njia za kuendeleza zao hilo.

Mwisho

No comments: