Monday, November 4, 2013

Maandalizi ya mkutano ya majadiliano ya wawekezaji na serikali yaendelea vizuri—TNBC



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Maandalizi ya mkutano ya majadiliano ya wawekezaji ya kitaifa na kimataifa kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine inayotarajiwa kufanyika mwezi huu inaendelea vizuri.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Bw. Raymond Mbilinyi aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa Kinachofanyika sasa ni maandalizi ya mada ya nini kitazungumzwa wakati wa mkutano.
TNBC ndio wanaoratibu mkutano huo.
“Mada ya kwanza ni mazingira ya biashara…kuna kikundi kazi kinachotayarisha mada hii kwa kuangalia maeneo yanayotakiwa kuboreshwa na serikali ili sekta binafsi iweze kufanya biashara vizuri,” alisema Mbilinyi. 
Alisema kikundi kazi hicho kinachoundwa na wadau toka sekta binafsi na umma sasa kinapitia maeneo mbalimbali ambayo ni muhimu kujadiliwa na pia kuangalia ripoti mbalimbali za kimataifa zinavyoonyesha jinsi Tanzania inavyopimwa.
“Kuna maeneo tunayofanya vibaya lakini pia kuna maeneo tunayofanya vizuri.  Sekta binafsi itakuja na mapendekezo yake na kujadiliana na sekta ya umma na kisha kuangalia jinsi ya kuboresha maeneo hayo,” alisema Mbilinyi. 
Alisema eneo la pili linalotarajiwa kuongelewa ni mpango wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’ ambalo serikali imejipima na kujipanga vizuri kufikia uchumi wa kati mwaka 2025. 
“Moja ya mambo yatakayojadiliwa ni ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza vipaumbele katika mpango huu wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’. 
Mkakati huo uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi Februari mwaka huu unalenga kufikia malengo katika vipaumbele vya maendeleo ya nchi kwa muda maalum ambapo viongozi wanatakiwa kuonyesha walichofanikisha.
Vipaumbele vya mkakati huo wa serikali ni pamoja na elimu, nishati, kilimo, usafiri, maji na maendeleo ya raslimali watu.
Kwa mujibu wa Bw. Mbilinyi eneo lingine litakalozungumziwa ni eneo la uwezeshaji kwa mapana yake. 
“Sekta binafsi ni kubwa nchi hii.  Tutaangalia utaratibu gani serikali iweze kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kuwa swala zima la maendeleo na uchumi linahusisha uwezeshaji,” alisema.
Mikutano hiyo ilianza kufanyika mwaka 2003 ikishirikisha wawekezaji wa ndani na wa nje kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine kwa malengo ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kwa manufaa ya pande zote mbili.
Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ndilo lenye dhamana ya uandaaji wa mikutano hiyo kwa miaka 10 sasa.
Mikutano hii ilianzishwa kuwa kama jukwaa la kubadilishana uzoefu katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Mwisho

No comments: