Monday, November 11, 2013

Sekta binafsi yakaribisha wenzao wa ulaya

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Sekta binafsi Tanzania imewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi za Ubelgiji, Ugiriki na Italia na kusema kuwa itawapa ushirikiano unaotakiwa kwa faida ya pande zote mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye alisema hayo wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika kwa heshima ya ugeni wa wafanyaiashara 65 toka nchi hizo tatu wanaotembelea Tanzania kuangalia fursa.
Chakula hicho kilitayarishwa na TPSF mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Bw. Simbeye alisema kama kiunganishi cha sekta binafsi Tanzania, TPSF iko tayari kufanya kazi na wafanyabiashara hao kwa faida ya Tanzania na nchi zao pia.
“Hii ni neema kwa nchi yetu…ni lazima tuitumie nafasi hii,” alisema.
Alisema TPSF ni chombo imara kinachowakilisha sekta binafsi Tanzania na kwamba kwa kufanya nacho kazi, wawekezaji hao watajihakikishia faida hapa nchini na kurahisisha kazi zao.
Aliwaambia kuwa Tanzania imeweka mfumo mzuri wa wawekezaji na wafanyabiashara kuwasiliana na serikali na kuelezea mawazo yao, mazingira aliyosema kuwa ni faida kwa wale wanaotaka kuja kuwekeza na kufanya biashara Tanzania.
“Mikutano ya majadiliano kati ya serikali na wawekezaji inatoa nafasi nzuri kwa sekta binafsi kutoa mchango wao katika maamuzi yanayowagusa,” alisema.
Hata hivyo, alitoa changamoto kwa kampuni za hapa nchini kuhakikisha kuwa zinajitahidi kufikia viwango vinavyotakiwa ili kuweza kuvutia na kujenga ushirika na kampuni za kimataifa.
Akiongea katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule aliyekuwa mgeni rasmi alisema serikali iko tayari kufanya kazi na wawekezaji toka nchi hizo na kuwa mazingira yanaridhisha.
“Hii ni fursa nzuri ya sisi kujenga mahusiano imara na wawekezaji hawa,” Bw. Haule aliyemuwakilisha Waziri wake Bernard Membe alisema.
Alisema sera ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali (PPP) hapa Tanzania inatoa nafasi kwa serikali kufanya kazi vizuri na sekta binafsi.
Alimpongeza Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya (EU), Dkt. Diodorus Kamala kwa kutayarisha na kufanikisha ujio huo.
“Tunakushukuru na kukupongeza kwa juhudi zako…tuna imani utaendeleza juhudi hizo,” alisema.
Kwa mujibu wa Dkt. Kamala juhudi hizo ni mwanzo wa kutekeleza sera mpya ya serikali ya mambo ya nje ya diplomasia ya uchumi.
Dkt. Kamala alisema kuwa sera hiyo, pamoja na mambo mengine, inalenga kuvutia zaidi uwekezaji, kuuza zaidi bidhaa nje, na kukuza utalii.
“Tunataka kuimarisha mahusiano na nchi hizi kwa faida ya pande zote,” alisema.
Alisema kuwa ubalozi wake mjini Brussels uko katika hatua za mwisho kutayarisha mpango mkakati wa jinsi ya kutekeleza sera hiyo ya diplomasia ya uchumi na kwamba mpango ni kuleta ujumbe wa watu 100 kila mwaka toka Ubelgiji na nchi nyingine za EU kuja kuangalia fursa hapa nchini.
Mkuu wa msafara wa wafanyabiashara hao, Bw. Malin Johan alisema ujumbe huo una wataalamu mbalimbali kama katika maeneo ya bandari, nishati endelevu, wahandisi, mafuta na gesi na kilimo.
Kabla ya kufika Tanzania, ujumbe huo ulizuru nchi ya Kenya.
Wanategemea kuondoka Jumatano ya wiki hii baada ya kutembelea visiwa vya Zanzibar.

Mwisho

No comments: