Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Asasi ya Kusaidia Uwekezaji Kwenye Kilimo (PASS Trust)
imesema itaendelea kutoa misaada katika Kilimo cha korosho ili wananchi wa
mikoa ya kusini ambao hutegemea zao hilo waweze kuondokana na hali duni ya
vipato.
Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi hiyo, Bw. Iddy Lujina
aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa wadau wa korosho jijini Dar es
Salaam hivi karibuni kuwa zao la korosho ni moja ya mazao ambayo yanahitajika
kupatiwa kipaumbele kwa maendeleo ya jamii.
“Asasi yetu imejidhatiti kuhakikisha zao hili linapiga
hatua,” alisema na kuongeza kuwa tayari wameshaanza kusaidia wakulima, viwanda
vya kusindika korosho na wasafirishaji kupata mikopo kuendeleza sekta ndogo ya
korosho.
Mikoa ya kusini inayozalisha zao la korosho ni pamoja
na Lindi, Mtwara, Pwani na wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Aliongeza kusema kuwa hadi sasa wameshasaidia wakulima
wa mikoa hiyo kupata mikopo kwa ajili ya kununua pembejeo, malori ya
usafirishaji mazao na matrekta kwa ajili ya kilimo.
Pia wametoa mikopo ya kwa ajili ya ujenzi wa maghala
ya mazao, na kwa ajili ya kununua mazao yanayoenda katika masoko ya nje.
Kutokana na mchango wake, PASS ilikuwa moja ya taasisi
zilizoshirikishwa katika mkutano huo wa wadau wa korosho.
Alisema Asasi yao imefungua tawi Mtwara kwa ajili ya
kuhudumia wakulima wa kanda hiyo kupata msaada wa mikopo kuendeleza Kilimo
likiwemo zao hilo.
Alisisitiza kuwa wakulima nchini wanahitaji kuwezeshwa
kwa vile asilimia kubwa ya watanzania hutegemea shughuli za Kilimo kujipatia
vipato.
“Zao la korosho soko lake ni kubwa hivyo Kilimo hicho
kipatiwe vipaumbele kwa lengo la kufikia malengo yake,” alisema.
Aliendelea kusema kuwa misaada wanayoitoa ni moja ya
hatua za kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali za kuendeleza Kilimo hapa
nchini.
“Mikati ya serikali ya matokeo makubwa sasa na mipango
ya kufikia uchumi wa kati inatakiwa kwenda sambamba na mipango ya kukiwezesha
Kilimo kukuwa,” alisema.
Hivi karibuni wadau wa sekta ndogo ya korosho
walikutana jijini Dar es Salaam kujadili maswala mbalimbali ya kukuza zao hilo
katika mnyororo wake.
Kupitia huduma zake, mwaka 2011 PASS ilisaidia wakulima 11,000
kupata mikopo yenye thamani ya Tshs 22 bilioni kutoka kwenye benki mbalimbali
na mikopo hiyo ilipanda hadi kufikia Tshs 30 bilioni mwaka jana.
Hadi sasa, taasisi hiyo ina matawi katika mikoa ya Morogoro,
Mbeya, Dar es Salaam, Mwanza, Moshi na Mtwara.
Katika miaka kumi iliyopita, PASS imeweza kusaidia wakulima zaidi
ya 100,000 kupata mikopo na katika mpango wake mpya wa miaka mitano inatarajia
kusaidia wakulima zaidi ya 300,000 kuweza kupata mikopo yenye thamani ya Tshs
290 bilioni.
PASS ilianzishwa mwaka 2000 chini ya mpango wa
uendelezaji sekta ya kilimo(ASPS) kwa msaada kutoka serikali ya Kifalme ya
Denmark kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwisho
No comments:
Post a Comment