Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imetambua mchango wa Mamlaka ya Uwekezaji katika
kanda maalumu (EPZA) katika uendelezaji sekta ya viwanda hapa nchini.
Mchango huo umetambuliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
alipokuwa akifungua maadhimisho ya siku ya viwanda Afrika jijini Dar es Salaam
hivi karibuni.
Waziri Mkuu Pinda alisema katika kuimarisha mafanikio na
juhudi hizo, serikali itaendelea kusimamia uwekezaji katika maeneo maalum ya
uzalishaji ili kuharakisha maendeleo ya viwanda nchini.
“EPZA inaendeleza kwa kasi kuhamasisha ukuaji wa viwanda
kupitia maeneo maalumu ya uwekezaji,” alisema.
Alifafanua kuwa katika juhudi hizo, katika kipindi cha miaka
sita iliyopita mamlaka hiyo imeanzisha viwanda
81 katika maeneo mbalimbali nchini.
“Viwanda hivi vimewekeza mtaji wa zaidi ya Dola za Kimarekani
Bilioni 1.12 na vimetoa ajira za
moja kwa moja 27,000 na zisizo
za moja kwa moja zaidi ya 80, 000,”
alisema.
Alisema kuwa mauzo nje kutokana na uwekezaji katika maeneo ya
mamlaka hiyo yamefikia Dola za Marekani Milioni
700.
“Serikali inaendelea kuimarisha EPZ ili iweze kuwa kichocheo
cha kukuza uchumi nakujenga ajira kupitia maendeleo ya viwanda,” alisema.
Waziri Pinda alitoa wito kwa wawekezaji zaidi wa ndani na nje
kuchangamkia uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji (SEZ) na Maeneo ya
Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ).
Alisema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa uendelezaji wa maeneo
ya EPZ na SEZ ni moja ya mikakati ya kukuza ajira, uwekezaji na kufikia
maendeleo endelevu kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, msukumo mkubwa uliowekwa na
serikali ya awamu ya nne katika kuendeleza Viwanda ilikuwa ni pamoja na
uanzishwaji na uendelezaji wa Maeneo ya Fursa huru za Uwekezaji kama Mamlaka ya
Maeneo Huru ya Uzalishaji kwa mauzo Nje (EPZA) na SEZ.
Alifafanua kuwa kati ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa
na serikali katika kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika Uwekezaji na
biashara katika soko la ushindani ni pamoja na kuipa nguvu ya kisheria mamlaka
ya maeneo huru ya uzalishaji kwa mauzo nje (EPZA) kusimamia uwekezaji katika
maeneo maalum ya uwekezaji (SEZ).
“Katika maeneo hayo, wawekezaji wa sekta mbalimbali
wataweza kuzalisha na kuuza bidhaa katika masoko ya ndani na nje ya nchi,”
alisema.
Alisema serikali kupitia EPZA kwa kushirikiana na serikali za
mitaa, inaendelea na jitihada za kutenga maeneo maalum ya uwekezaji katika
mikoa iliyobaki ya Simiyu, Katavi, Geita na Njombe.
Akielezea umuhimu wa kuendeleza sekta ya viwanda, Waziri Mkuu
alisema sekta hiyo ina jukumu kuu la kuleta mabadiliko ya kuitoa nchi katika
uchumi ulio nyuma na tegemezi na kufikia kiwango cha uchumi wa Kati wa Viwanda
unaoongozwa na kilimo cha kisasa na cha kibiashara chenye tija kama
inavyofafanuliwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya hadi 2025.
Alisema utekelezaji wa jukumu hilo utaongeza kasi ya ukuaji
wa uchumi, kuongeza ajira, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za
viwandani, zinazokidhi mahitaji ya Wananchi na kuwepo kwa uchumi endelevu.
Kwa mujibu wa takwimu, mchango wa Sekta ya Viwanda katika
Pato la Taifa (GDP), uliongezeka kutoka asilimia 9.6 mwaka 2010/2011 na kufikia Asilimia 9.9 mwaka 2011/2012 wakati mchango wa bidhaa za viwandani katika
mauzo ya nje uliongezeka kutoka asilimia 16.9 mwaka 2011 hadi Asilimia 17.7 mwaka 2012.
Ajira za moja kwa moja kwenye sekta hii ziliongezeka kutoka
wafanyakazi 115,022 mwaka 2011
hadi wafanyakazi 120,840 mwaka
2012.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya viwanda Afrika ilikuwa: “Ajira
na Ujasiriamali: Fursa ya Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika.’
Mwisho
No comments:
Post a Comment