Wednesday, November 13, 2013

TCCIA kufanya mkutano mkuu kesho



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya TCCIA Investment Company LTD (TCCIAIC) inatarajia kufanya mkutano wake mkuu wa mwaka kesho.
Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa TCCIA Investment Company LTD, Bw. Donald Kamori alisema mkutano huo mkuu wa nane wa wanahisa utakaofanyika jijini humo unatarajiwa kuhudhuriwa na wanahisa wake waliotapakaa nchi nzima.
“Wanahisa wa kampuni hii watapata taarifa ya nini kimefanyika katika mwaka mmoja uliopita na mipango ijayo,” alisema Bw. Kamori.
Pamoja na taratibu nyingine za kawaida, mkutano huo utapokea na kuridhia taarifa ya wakurugenzi kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 31 Disemba 2012 pamoja na taarifa ya hesabu za kampuni za mwaka wa fedha zilizokaguliwa katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa Bw. Kamori mkutano huo pia utapokea na kuridhia pendekezo la bodi kulipa gawio la mwisho kwa mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2012 na pia gawao la awali kwa mwaka wa fedha unaoishia Disemba 2013.
Pia mkutano huo utapokea na kuridhia pendekezo la malipo ya wakurugenzi wa bodi wa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa Bw. Kamori, mkutano huo pia utapokea na kuridhia pendekezo la bodi kuhusu uteuzi wa mkaguzi wa hesabu za kampuni kwa mwaka wa fedha utakaoishia Disemba 31, 2013.
Pia mkutano utapokea na kuridhia mapendekezo ya bodi ya kuanza mchakato wa kuuza hisa na kujiunga na soko la hisa la Dar es Salaam.
TCCIAIC ni kampuni iliyoanzishwa Chama cha Watanzania wanaojishughulisha na Biashara, Kilimo na Viwanda (TCCIA) katika kutetea, na Kulinda haki zao kwa pamoja kwa maslahi ya watanzania na taifa kwa ujumla.
Mtaji wa kampuni hiyo umekuwa toka shilingi bilioni 2.3 mwaka 2008 na kufikia shilingi bilioni 6.3 mwishoni mwa mwaka 2012.
Mwisho

No comments: