Friday, November 15, 2013

RUBADA yatoa somo kwa vijana kambi ya kilimo ya Mkongo



Na Mwandishi wetu, Rufiji

Vijana katika kambi ya Kilimo na maarifa ya Mkongo wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani wametakiwa kujituma katika mafunzo yao ili waende kuwa mabalozi wazuri katika sekta ya kilimo kwenye vijiji vyao.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja alitoa changamoto hiyo alipowatembelea vijana hao kuangalia maendeleo na changamoto mbalimbali zilizopo tangu kuzinduliwa kwake na Rais Jakaya Kikwete mwezi Octoba mwaka huu.

“Mnatakiwa kuwa mfano wa kuigwa mara mtakapomaliza mafunzo haya,” aliwaasa vijana hao hivi karibuni.

Aliwatahadharisha vijana hao kutojenga dhana ya kupata ajira pindi watakapomaliza mafuzo yao katika kambi hiyo, ambayo lengo lake kubwa ni kuwaweka vijana pamoja na kujifunza kilimo kwa vitendo na kuwa mfano kwa wengine.

“Msije mkajenga dhana ya kupata ajira mahala, mradi huu lengo lake ni kuwawezesha ninyi kujitegemea, mkawe mabalozi katika kata, vijiji na vitongoji vyenu, mnatakiwa kujituma sana pamoja na kufuata maelekezo ya walimu wenu,” aliongeza Bw. Masanja.

Alisema vijana hao wapatao 50 watagawanywa katika makundi mbalimbali kulingana na aina ya miradi iliyopo katika kambi hiyo kama vile kilimo cha mazao ya chakula, ufugaji, ukulima wa mbogamboga na usindikaji.

Alisema hadi kufikia katikati ya mwezi huu tayari vijana hao watakuwa wamepatiwa zana mbalimbali za kufanyia kazi ikiwemo trekta lililo kamilika kwa ajili ya kuanza kilimo katika eneo hilo la mkongo.

“Niwahakikishie tu kuwa tayari mpango wa kuwaletea trekta na vifaa vingine uko tayari, hivyo ni ninyi kuhakikisha kuwa mnazingatia yale mtakayoelekezwa na viongozi wenu katika kambi hii,” alisema.

Pia alisisitiza suala la nidhamu na uvumilivu miongoni mwa vijana katika kambi hiyo na kusema kuwa ni vigumu kufikia malengo wanayotaka kama hawatazingatia mambo hayo katika mafunzo yao.

Kwa upande wake Mkuu wa kambi hiyo ya vijana, Bw. Itunda Mbwambo, alimhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa vijana hao wako vizuri kiakili na kimwili katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika kambi hiyo.

“Nikutoe wasiwasi mkuu, hawa vijana wanajituma, wanafanya kazi, wanafuatilia mafunzo vizuri, hivyo ni matumaini yangu baada ya kipindi kilichowekwa watakuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii,” alisema Bw. Mbwambo.

RUBADA inatarajia kuzalisha vijana 600 kutoka kituo cha Mkongo hadi 2015 ambao watakuwa na utaalamu na ujuzi wa kilimo chenye tija na ufugaji wa kisasa.

Kilimo ni moja ya sekta zinazolengwa katika mikakati mbalimbali ya serikali katika mapinduzi ya kiuchumi na kufikia malengo ya Milenia na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

Kulingana na sensa ya watu ya 2012, asilimia 60 ya nguvu kazi ya Tanzania ni vijana.

Mwisho  

No comments: