Sunday, November 10, 2013

TCME yakanusha kampuni za madini kuishtaki serikali ICC



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Jumuiya ya Wachimba Madini na wazalishaji Nishati Tanzania (TCME) imesema imesikitishwa na kushtushwa na taarifa iliyotolewa na gazeti moja la kila siku mapema wiki hii kuwa baadhi ya kampuni za madini zina mpango wa kuishtaki serikali kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Biashara yaani International Chamber of Commerce (ICC).

Kwa mujibu wa habari hiyo iliyotoka katika gazeti la kiingereza la The Citizen jumatatu wiki hii, makampuni hayo yanataka kuiburuza serikali ICC yakiwa na madai ya marejesho ya kodi yanayofikia dola za kimarekani 410 milioni.

“Tunakanusha habari hiyo iliyojaa uzushi na uongo,” inasomeka sehemu ya taarifa ya TCME iliyotolewa jana na kusainiwa na mwenyekiti wake, Bw. Joseph Kahama.

Katika habari hiyo inadaiwa kwamba kampuni kubwa za kimataifa zinazofanya kazi hapa nchini ikiwemo AnglogoldAshanti ya Afrika ya Kusini zina mpango wa kuipeleka serikali ICC kudai jumla ya USD 410 milioni (Tshs 676 bilioni) kama marejesho ya kodi wanayodai.

Habari hiyo pia inahusisha kampuni za Resolute Tanzania Ltd na African Barrick Gold.

Hata hivyo Bw. Kahama anasema hakuna afisa yeyote kati ya kampuni hizo zilizotajwa aliyehojiwa mbali na Africa Barrick Gold.

Kwa mujibu wa habari, maafisa waliohojiwa hawakupenda kutajwa majina.

“Hakuna chembe ya ukweli katika habari hii kwamba wanachama wetu wanataka kuipeleka serikali ICC,” alisema Bw. Kahama kwenye taarifa yake. 

Bw. Kahama alisema kwamba umoja wao unafahamu kuwa kuna matatizo na kutokuelewana kati ya kampuni za madini na idara mbalimbali za serikali kuhusu maswala kadhaa ambayo yamechukua muda mrefu na yasiyo na tija kwa pande zote mbili.

“Hata hivyo, tunaamini kuwa hakuna sababu ya kuamua kuchukua hatua kama hiyo ya haraka bila ya kuifahamisha kwanza serikali,” alisema na kuongeza kuwa wao siku zote wanahamasisha  ni uhusiano bora kati ya chombo hicho, wanachama na serikali.

Alisema kwamba kama ingeamuliwa kuchukuliwa hatua kama hiyo, tathmini kubwa kuangalia faida na hasara ingefanyika na kwamba TCME huzingatia maadili katika biashara ikiwa inashughulikia maswala nyeti kama hayo.

“Hatua hizo zingehusisha mijadala na mazungumzo kabla ya kuchukua hatua kubwa zaidi,” alisema.  

Alisema chombo hicho na wanachama wake wataendelea kuwa na mahusiano mazuri yaliyopo kati yao na serikali ili kuhakikisha kuwa uwekezaji zaidi katika sekta ya madini unafanyika na kuendelea kuwa chanzo cha mapato ya serikali.

Alisema muda umefika kwa serikali kuchukua hatua muhimu kushughulikia matatizo mbalimbali yanayohusu sekta ya madini na kampuni za madini.

Alisema moja ya swala linalopaswa kushughulikiwa sasa ni marejesho ya VAT ambayo kwa sasa yanaelekea kuwa mamilioni ya dola za kimarekani,” alisema, na kuongeza kuwa hali hii inatokea sasa ambapo bei ya dhahabu imeshuka hadi dola 1,300 kwa kilo kutoka dola 1,800 kwa kilo.
“Hali hii imesababisha matatizo makubwa ya mzunguko wa fedha katika kampuni hizi,” alisema.
Mwisho  

No comments: