Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imsema inaendelea na mchakato wa majadiliano
na Kampuni ya Simu za Mikononi ya Airtel kuiwezesha serikali kumiliki hisa zote
za Kampuni ya Mawasiliano ya (TTCL).
Naibu wa Waziri, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Bw. January Makamba alisema wakati akifunga Kikao cha Baraza Kuu la
Wafanyakazi wa TTCL jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa ni nia ya serikali
kuona inaimiliki TTCL kwa asilimia 100.
“Kwa sasa shirika hili lina miundombinu yote na uwezo
wa kufanya kazi vyema,”alisema.
Kwa sasa kampuni ya Airtel inamiliki asilimia 65
wakati TTCL inamiliki asilimia 35.
Aliongeza kusema kuwa ni dhamira ya wizara na serikali
kwa ujumla kuona TTCL inashika hatamu katika kuongoza sekta ya mawasiliano hapa
nchini ili kufikisha huduma hiyo sehemu zote za nchi.
Aliitaka kampuni hiyo kuingia katika teknolojia ya
masafa ya GSM ambayo yanawezesha wateja wake kutumia simu moja kwa laini zaidi
ya moja tofauti na teknolojia inayoyotumika sasa ya CDMA ambayo inatumia laini
moja tu.
Alisisitiza kwamba serikali itaiwezesha kampuni kupata
mkopo kwa ajili ya kufikia malengo yake hayo ili kuzidi kutoa huduma bora kwa
watanzania.
Pia alipongeza kampuni hiyo kwa kutoa huduma bora ya
mkongo na aliagiza uongozi kuzidi kuutunza na kutafuta masoko zaidi ili watu
wazidi kupata hudma za mawasiliano yakiwemo ya intaneti kwa ufanisi na urahisi.
Aliwaambia wafanyakazi kuwa historia ya kampuni hiyo
kufanya vibaya huko nyuma sasa ni historian a kuwataka kufanya kazi kwa bidii
na kwa kufuata sheria zilizopo.
“Ninaamini tunaweza kufanya vema zaidi ya tulivyo
fanya nyuma...ni dhamira ya serikali kufikia azma hiyo,” alisema na kuongeza
kuwa TTCL ina kila sababu za kuongoza sekta ya mawasiliano hapa nchini.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu TTCL, Dkt.
Kamugisha Kazaura alisema mpango mkakati wa Kampuni wa miaka mitatu 2013-2015
ni kutekeleza miradi kwa kuongezwa tija na ufanisi.
“Kampuni imedhamiria kuboresha mapato kutoka Tshs
bilioni 92.3 mwaka 2012 hadi Tshs bilioni 111.8 mwaka 2014,” alisema.
Aliongeza kuwa pia wamepanga kuongeza idadi ya wateja
wa huduma mbalimbali za simu, sauti na data.
Alisema pia wanatarajia kuboresha makusanyo ya mapato
na madeni ya kampuni yanayotokana na huduma za simu zinazotolewa kila mwezi kwa
wateja wake, ikiwemo serikali kuu na taasisi zake.
Alisisitiza kuwa katika mpango mkakati wa kibiashara wa mwaka 2014 -2016 kampuni imedhamiria kujizatiti zaidi katika nyanja ya
huduma za intaneti na pia kuingia kwa dhati katika ushindani wa soko la
simu za mkononi kwa kutumia teknolojia ya 4G LTE na GSM.
Alisema kampuni inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha za kutosha kuwezesha kampuni
kujipanua kibiashara, ushindani wa kibiashara na hujuma ya mtandao.
Kikao Kikuu cha baraza la wafanyakazi kilikuwa cha
siku tatu na kuhusisha wajumbe wake toka nchi nzima kujadiliana maswala
mbalimbali ya kuendeleza kampuni hiyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment