Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA)
imesema iko tayari na inawakaribisha wawekezaji toka nchi za ulaya kuwekeza
katika maeneo yake.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru
aliwaambia waandishi wa habari hivi karibuni kuwa maeneo maalumu ya mamlaka
hiyo yanatoa fursa nzuri kwa wawekezaji hao kufaidika na uwekezaji wao hasa
katika maeneo ya viwanda.
Dkt. Meru alikua akiongea mara baada ya kumalizika kwa
kongamano lililohusisha wafanyabiashara wa Tanzania kwa upande mmoja na wenzao
kutoka na nchi za Ubelgiji, Italia na Ugiriki lililofanyika jijini humo hivi
karibuni.
“Tunawakaribisha kuwekeza katika maeneo yetu na tuko
tayari kufanya nao kazi,” alisema.
Alisema mamlaka yake iko katika jitihada za kuongeza
zaidi maeneo ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi toka ndani na nje
ya nchi.
Alisema ujio wa wawekezaji hao unafungua sura mpya ya
mahusiano na nchi za ulaya ambazo miaka ya nyuma zilikuwa mshiriki mzuri kwenye
uwekezaji Tanzania.
“Ujio huu unafungua ukurasa mpya wa mahusiano ya
kibiashara na Tanzania ipo tayari kushirikiana nao,” alisema.
Alisema kwa sasa Tanzania ni nchi inayovutia nchi
kubwa kuja kuwekeza kutokana na juhudi za Rais Jakaya Kikwete kuitangaza nchi
nje na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Rais Jakaya Kikweze anastahili kupongezwa kwa kazi
anayoifanya kwa sababu kukaribisha wawekezaji ni kupanua wigo wa walipa kodi
hapa nchini,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye alisema sekta binafsi iko
tayari kufanya kazi na wawekezaji hao.
Bw. Simbeye alisema kama kiunganishi cha sekta binafsi
Tanzania, TPSF iko tayari kufanya kazi na wafanyabiashara hao kwa faida ya
Tanzania na nchi zao pia.
“Hii ni neema kwa nchi yetu…ni lazima tuitumie nafasi
hii,” alisema.
Alisema TPSF ni chombo imara kinachowakilisha sekta
binafsi Tanzania na kwamba kwa kufanya nacho kazi, wawekezaji hao watajihakikishia
faida hapa nchini na kurahisisha kazi zao.
Aliwaambia kuwa Tanzania imeweka mfumo mzuri wa
wawekezaji na wafanyabiashara kuwasiliana na serikali na kuelezea mawazo yao,
mazingira aliyosema kuwa ni faida kwa wale wanaotaka kuja kuwekeza na kufanya
biashara Tanzania.
Alitoa changamoto kwa wafanyabiashara wa Tanzania
kuhakikisha wanahudhuria makongamano kama hayo maana ni fursa ya kujenga
mahusiano ya kibiashara.
“Wafanyabiashara wajenge utamaduni wa kuhudhuria
makongamano kama haya...hii ni kwa faida yao na ya nchi pia,” alisema.
Mwisho
No comments:
Post a Comment