N a Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wafanyabiashara wa Tanzania wamehamasishwa kutumia
fursa za kibiashara kuwekeza nchini Botswana hasa baada ya nchi hiyo kufungua
ubalozi mdogo hapa nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bw. Bernard Membe alisema wakati akifungua ofisi hiyo ya ubalozi mdogo jana
jijini Dar es Salaam kuwa sasa ni wakati mwafaka kwa wafanyabiashara
watanzania kuitumia ofisi hiyo kuimarisha biashara zao na uhusiano na wenzao
toka nchi hiyo.
Ufunguzi wa ofisi hiyo unakuja miezi saba baada ya
nchi ya Botswana kumteuwa Mtanzania, Bw. Emmanuel Ole Naiko kuwa balozi wa
heshima anayeiwakilisha nchi hiyo hapa Tanzania.
“Pamoja na mambo mengine, ofisi hii sasa itatumika
katika kuwaunganisha wananchi wa nchi hizi hasa katika maswala ya biashara na
uwekezaji,” alisema Waziri Membe.
Alisema uhusiano wa Tanzania na Botswana ni wa
kihistoria tangu miaka ya 60 wakati waasisi ya nchi hizo walipofanyakazi pamoja
katika kupigania uhuru na maendeleo ya nchi zao.
“Hatua hii ni uthibitisho wa uhusiano wa kihistoria
uliopo kati ya nchi hizi,” alisema.
Alitaja maeneo ambayo nchi hizo zinaweza kushirikiana
kama kuendeleza wananchi wa pande hizo kama madini, Kilimo, ufugaji na utalii
na nyingine.
Awali nchi hiyo haikuwa na Balozi nchini Tanzania,
badala yake ilikuwa ikimtumia Balozi wa Zambia kushughulikia maswala yake hapa
nchini.
“Hakuna ulazima wa watanzania kuomba visa kwenda
Botswana...tuitumie nafasi hiyo kwa maendeleo,” alisema.
Kwa upande wake, Bw. Ole Naiko alisema ofisi hiyo
inakaribisha wafanyabiashara wa nchi zote mbili kuitumia na kutafuta fursa
zilizopo katika nchi zote ili kukuza biashara na uwekezaji.
“Nchi hizi zina mambo ambayo kilamoja inaweza kufanya
kwa ufanisi...tukiunganisha nguvu zetu tutaweza kusonga mbele kwa mafanikio,”
alisema.
Alisema Botswana imepiga hatua kubwa katika kuongeza
thamani ya madini yake na kwamba hilo ni eneo moja ambalo Tanzania inaweza
kujifunza ili kufaidika na madini yake.
“Tukishafahamu wenzetu wanafanya nini katika kuongeza
thamani madini yao tujifunze na kutumia maarifa hayo katika sekta nyingine kama
kilimo,” alisisitiza.
Alisema kufikia malengo hayo kunahitajika kuzidi
kuongeza misingi ya utawala bora na kupiga vita rushwa, vitu ambavyo
vinarudisha nyuma harakati za maendeleo.
Naye Balozi wa Botswana nchini Zambia na Tanzania, Bi.
Tuelonyana Oliphant alisema nchi yake inayo furaha kufungua ubalozi mdogo
nchini Tanzania.
“Kwa niaba ya serikali ya Botswana, natoa shukrani kwa
serikali ya Tanzania kuturuhusu kufungua ofisi hii,” alisema.
Nchi ya Botswana imepakana na nchi za Afrika ya
Kusini, Zimbabwe, Namibia na Zambia. Ina ukubwa wa Sq km 58,200, na wakazi
Milioni 2.
Ni nchi iliyo na amani na utulivu toka uhuru na ina
kiwango kidogo sana cha rushwa barani Afrika.
Nchi hiyo imedhamiria kuongoza katika sekta za fedha,
madini hasa Uranium, shaba na usafirishaji wa almasi, na Copper na pia
kuendeleza uwekezaji katika sekta ya utalii kwani Botswana ina mbuga nyingi za
wanyama na hasa Vistoria Falls ambayo iko mpakani na Zimbabwe na Zambia katika
mji wa Kasane.
Mwisho
No comments:
Post a Comment