Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji
na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu (wa pili kulia) akifuatilia jambo wakati
wa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao kutoka nchi za Ubelgiji,
Italia na Ugiriki lililofanyika jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni Balozi wa
Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya (EU), Dkt. Diodorus Kamala (kulia),
Balozi wa Ubelgiji hapa nchini, Bw. Koen Adam (kushoto) na Naibu waziri wa Biashara na Viwanda, Bw.
Gregory Teu (wa pili kushoto).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu
akiteta jambo na Balozi wa wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya (EU), Dkt.
Diodorus Kamala wakati wa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao
kutoka nchi za Ubelgiji, Italia na Ugiriki lililofanyika jijini Dar es Salaam
jana.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wafanyabiashara nchini wameshauriwa kuchangamkia fursa za
uwekezaji kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka nje ya nchi ili waweze kupata
ujuzi,mitaji na teknolojia.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na
Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu amesema kuna faida wafanyabiashara wa Tanzania
wakiwekeza kwa ushirkiano na wafanyabiashara wa nje na kwamba utaratibu huu
umefaidisha mataifa mengi.
Dkt. Nagu alikuwa akiongea na waandishi wa habari
katika kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania, na ujumbe wa wafanyabiashara
kutoka Italia, Ubelgiji na Ugiriki.
Kongamano hilo lilitayarishwa na Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC).
“Serikali inapenda kuona wafanyabiashara wetu wanawekeza
kwa ushirikiano na wawawekezaji kutoka nje…kwa kufanya hivyo wafanyabiashara
wetu watapata ujuzi, mitaji na teknolojia,” alisema.
Alisema katika kuona jambo hilo linafikiwa, serikali
inafanya jitihada mbalimbali za kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na
wawekezaji kutoka nje ya nchi ili wazungumze biashara.
Alisistiza kuwa hatua hiyo pia ni moja ya jitihada za
kufikia mkakati wa Matokeo Makubwa sasa (BRN) na kufikia uchumi wa kati 2025
kwa mujibu wa dira ya taifa ya maendeleo.
Alisema sekta binafsi imeachiwa kusimamia na kuendesha
uchumi, hivyo itumie nafasi ya ujio wa wafanyabiashara hao kujenga mahusiano ya
kikazi ya kudumu kwa faida ya pande zote mbili.
Aliwashauri wafanyabiashara wazalendo waungane pamoja
kujenga makampuni makubwa na kutumia umoja wao kukopa fedha kutekeleza miradi
mikubwa ili nchi ifaidike zaidi na rasirimali za nchi.
Akifafanua zaidi alisema hata wawekezaji kutoka nje
wanaokuja kuwekeza Afrika, makampuni yao ni ya watu waliounganisha nguvu,
mitaji na wanakopa fedha kwenye taasisi za fedha na kupanua biashara zao.
Balozi wa Ubelgiji nchini, Bw. Koen Adam alisema
wafanyabiashara waliokuja kutoka katika nchi hizo tatu wanatoka katika
makampuni makubwa ambayo yana uwezo mkubwa kiuwekezaji.
“Ninatambua Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu na
rasirimali nyngini, hivyo inaweza kufaidika zaidi kama sekta binafsi itajenga
uwezo kwa kushirikiana na wenzao kutoka nje,” alisema.
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya
(EU), Dkt. Diodorus Kamala alisema nia ya kuwaleta wafanyabiashara wa nchi
hizo, ni kuwakutanisha na wenzao wa Tanzania ili washirikiane kibiashara na na
kwamba wao wamebobea katika maswala mbalimbali na kuwa na ujuzi ambao unatakiwa
hapa nchini.
“Pande zote mbili zinaweza kufaidika kama zitashirikiana
vizuri,” alisema, na kutoa changamoto kwa watanzania kujenga uwezo wa kufanya
biashara za kimataifa.
Alisema Jumuiya ya Ulaya inaihitaji sana Afrika kuliko
wakati wowote na Afrika pia inaweza kufaidika na jumuiya hiyo.
“Watanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa kama hizi,”
alisema.
Mkurugenzi wa Huduma za Wawekezaji, TIC, Bi. Nakuala
Senzia alisema kituo chake kilitumia fursa ya ujio wa wafanyabiashara hao
kutangaza fursa za zinazopatikana hapa nchini.
“Tunahamasisha wafanyabiashara wa ndani na nje kuja
kuwekeza katika sekta mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa aliyetayari
kuwekeza hupatiwa vivutio vitolewavyo na kituo chake.
Alisema TIC mbali na kutoa vivutio hivyo pia husaidia
wawekezaji kupata vibali mbalimbali na kwa muda mfupi ili waweze kujenga uwezo
zaidi wa kufanya biashara hapa nchini na badaye kuwa walipa kodi wazuri.
Alisema nchi ikipata wawekezaji wengi itapanua wigo wa
walipa kodi na kuweza kufanya shughuli za maendeleo kwa haraka zaidi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment