Monday, November 4, 2013

Ole Naiko atoa changamoto kupata mitaala itakayowezesha wahitimu kujiajiri



Na Mwandishi wetu, Monduli
Serikali imeombwa kuharakisha kazi ya kutayarisha mitaala ya shule za msingi, sekondari, vyuo vyote vya mafunzo na vyuo vikuu ili kupata kada ya watu wanaoajirika baada ya kuhitimu mafunzo husika.
Wito huo umetolewa na mtumishi wa siku nyingi mstaafu wa umma, Bw. Emmanuel Ole Naiko alipokuwa akiongea kama mgeni rasmi katika mahafali ya 31 ya shule ya sekondari ya Moringe Sokoine, wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha mwishoni mwa wiki.
Bw. Ole Naiko ambaye pia ni balozi wa heshima wa Botswana nchini Tanzania alisema ni ukweli usiofichika kwamba mitaala inayotumiaka hivi sasa kufundisha vijana mashuleni haisaidii kutoa kada ya watu wanaoajirika katika soko la sasa la ajira.
“Licha ya kutishwa na uwingi wa Division Zero, idadi kubwa ya wanaomaliza shule ngazi zote hawana uwezo wa mawasiliano wala utaalamu wowote ule unaohitajika na soko la sasa,” alisema.
Alieleza kuwa hali hiyo ni kinyume kabisa na enzi za zamani ambapo kijana alipokuwa anamaliza elimu ya msingi wakati huo alikuwa anaweza akajiajiri mwenyewe kwa kuwa Fundi, Mwimbaji, Mcheza Senema ama Mzungumzaji anayejua kujenga hoja.
“Hii ina maana kwamba wahitimu wa wakati huo walikuwa wanaajirika kwani walikuwa na utaalam unaotakiwa na soko,” alisema.
Alisema sasa ni lazima kukubali kwamba kama jamii watanzania hawawezi kusitisha mchakato na mikakati ya Utandawazi ili manufaa yake yawafikie watu wengi zaidi na athari zake kwa nchi zipungue.
“Moja ya kujifunza kwa waliotumia utandawazi ni kutafsiri kwa hali halisi fursa zake katika hali ya nchi yetu,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa mambo watanzania wanayoweza kujifunza ni ubunifu wa namna ya kuvutia uwekezaji; kujenga utawala bora; kuwa wabunifu; kuwa wajasiriamali; kusaidia nchi yetu kisimamia uchumi wa soko; kubuni njia za kusaidia wananchi walio katika sekta isiyo rasmi waingie kwenye sekta rasmi, na mengine mengi.
“Nchi ya mfano wa kuigwa na jinsi ilivyofaidika na utandawazi ni nchi ya Malaysia. Ndiyo sababu nchi yetu imeamua kujifunza kutoka Malaysia jinsi kuendeleza uchumi watu kwa kuanzia na zile sekta tulizo na nguvu nazo,” alisema.
Alisema Malysia sasa ni moja ya nchi zilizoendelea na kwamba ni matumaini yake kwamba vijana wa Tanzania wakifundishwa vizuri zaidi namna ya kutumia utandawazi, watakuwa madereva wazuri wakuifikisha nchi kwenye mkakati wa Mtokeo Makubwa Sasa.
Eng. Ole Naiko ambaye alisoma katika shule hiyo miaka ya 1960 wakati huo shule hii ikiitwa Monduli Middle School aliwapongeza wahitimu kwa kufikia hatua hiyo ya awali ya matayarisho ya kujenga msingi wa maisha yao ya baadaye.
Aliwaasa wahitimu kutokubali kumaliza shule katika ngazi yeyote ile bila kuwa na ujuzi utakaowakufanya waajirike.
“Usikubali kuridhika na elimu hii ya wali uliyoipata; ichukulie kama ngazi ya kupanda kwenye ngazi nyingine kielimu na kitaalam,” aliwaambia.
Aliwaambia kwamba watambue kuwa mbele yao kuna hatari ya kupata magonjwa ya kila aina, lakini wanao uwezo wa kuepukana na maradhi hayo kwa kuzingatia maadili mema waliyofundishwa na wazazi, waalimu na viongozi wao wa dini.
Katika kuisaidia shule hiyo, Bw. Ole Naiko alianzisha kampeni ya kutafuta fedha za kununulia vitabu vya Sayansi na Arts.
“Najua Serikari itatoa fedha za kununua vitabu mwakani, lakini hazitoshi kwa hiyo naomba Bodi ituongoze jinsi wananchi wanaweza kuchangia mfuko wakununulia vitabu vya Sayansi na Arts vitavyowekwa maktaba,” alisema.
Yeye alianza na ahadi ya Tshs milioni 1.2 wakati Mbunge wa Monduli, Bw. Edward Lowassa alitoa ahadi ya Tshs 500,000.  Mfanyabiashara Shubash Patel alitoa ahadi ya Tshs milioni 1.
Mwisho

No comments: