Thursday, November 21, 2013

TCCIA Investment Company Limited yakuza mtaji wake maradufu

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCCIA Investment Company Limited (TCCIAIC), Mhandisi Aloys Mwamanga (katikati) akisisitiza jambo wakati wa mkutano mkuu wa nane wa kampuni hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Wengine ni makamu wake, Bw. Joseph Kahungwa (kushoto) na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Donald Kamori.

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
TCCIA Investment Company Limited (TCCIAIC) imetangaza kukuwa kwa mtaji wake kutoka Tshs. bilioni 8.39 Desemba 31, 2012 hadi kufikia Tshs bilioni 17.807 Novemba 12, 2013.
Mafanikio hayo yalitangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo, Mhandisi Aloys Mwamanga wakati wa mkutano mkuu wa nane wa kampuni hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Kwa mujibu wa Bw. Mwamanga, mafanikio hayo ni makubwa kupatikana ukilinganisha na miaka iliyopita.
“Mtaji wetu umeongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka 2013, na tunajipongeza kwa kazi nzuri,” alisema.
Alisema mafanikio hayo yamewezekana kutokana na bodi imara ya wakurugenzi, kamati bora ya uwekezaji na menejimenti makini.
Alisema uongozi huo umekuwa ukizingatia na kuweka kipaumbele kuiendeleza kampuni kwa kuwekeza katika makampuni yanayojiendesha kwa faida.
Pia alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji walioufanya kwenye makampuni tisa imara, yakiwemo ya NMB, CRDB, DCB, TBL, TCC Twiga, Simba, Swissport na Mwanza Community Bank.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo hiyo,Bw. Donald Kamori alisema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano mzuri wa utendaji kati ya menejimenti na bodi ya wakurugenzi.
Alisema kuwa mwaka ujao wa 2014 wamejipanga zaidi kuimarisha mtaji kwa kupanua uwezekezaji.
“Dhamira yetu ni kuwawezesha wanahisa kupata faida na kampuni kuzidi kujipanua,” alisema.
Alisema kwa sasa kampuni inajipanga kufanya tathimini na kuwekeza katika maeneo yatakayosaidia kupata faida zaidi yakiwemo majengo, na kuanzisha SACCOSS kama njia ya kuunga mkono serikali uwepo wa huduma za kibenki.
Njia nyingine kampuni inazofikiria ni pamoja na kuwekeza katika makampuni yaliyojiorodhesha katika soko la mitaji Dar es Salaam (DSE) na kununua hati fungani.
“Kampuni inajitahidi kuwekeza maeneo mbalimbali ili kuwa na uwigo mpana wa mapato na kuepuka hasara,” alisema.
Mkutano huo mkuu uliridhia taarifa mbalimbali zikiwemo utekelezaji maswala muhimu yaliyoamuliwa katika mkutano mkuu wa saba wa mwaka 2012.
TCCIAIC ni kampuni iliyoanzishwa Chama cha Watanzania wanaojishughulisha na Biashara, Kilimo na Viwanda (TCCIA) mwaka 1999 katika kutetea, na Kulinda haki zao kwa pamoja kwa maslahi ya watanzania na taifa kwa ujumla.
Mwisho

No comments: