Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kampuni toka nchini Singapore zimeonyesha
nia kubwa ya kuimarisha uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini zikwemo
raslimali za gesi na mafuta ambazo zinapatikana nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC), Bi. Juliet Kairuki aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari
kuna kampuni toka nchi hizo zilizokwisha nunua hisa kwenye vitalu vya mafuta na
gesi asilia.
Alikuwa akiongea baada ya hafla fupi ya
kutiliana saini ya makubaliano kati ya TIC na IE Singapore Cooperation
Enterprises toka nchi hiyo jana jijini Dar es Salaam.
“Tayari wengine wamesha nunua hisa kwenye
uwekezaji wa mafuta na gesi asilia,” alisema.
Makubaliano hayo yanahusisha kubadilishana
taarifa za uwekezaji kati ya Tanzania na Singapore kwa faida ya nchi zote
mbili.
Makubaliano hayo kati ya TIC na kituo
hicho toka nchini Singapore yalishuhudiwa pia kampuni nne toka nchi hiyo ambazo
zimekuja nchini kuangalia mazingira ya uwekezaji nchini ili waweze kuanza
kufuata taratibu za kuwekeza katika maeneo mbalimbali.
“Wamekuja kuangalia vivutio ambavyo
Tanzania inatoa ikiwemo vya uhamiaji, kodi, vibari vya wageni kufanya kazi
nchini, na ardhi kwa ajili ya uwekezaji,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa mahusiano hayo
yatasaidia kuendelea kuboresha maswala ya uwekezaji na kufanya biashara pamoja
na hiyo itawavutia wawekezaji wengi kutoka nchi hiyo kuja nchini.
Alisistiza kwamba Serikali inavutia
wawekezaji ili kupanua wigo wa kodi ili mapato ya nchi yaweze kuongezeka kwa
ajili ya ujenzi wa miundombinu ya nchi ambayo inachangia maendeleo.
“Kituo kipo tayari kusaidia kupitia
taratibu zake kuhamasisha na kuvutia uwekezaji zaidi nchini,” alisema.
Naibu Mwenyekiti, IE Singapore Cooperation
Enterprises, Bw. Seah Moon Ming alisema ujio wao nchini Tanzania unalenga
kuimarisha ushirikiano kati ya nchi yao na Tanzania katika nyanja za uwekezaji
na biashara.
“Tunataka kubadilishana taarifa za
kibiashara na uwekezaji kati ya nchi zetu ili kuleta maendeleo yetu sote,”
aliongeza kusema Bw. Moon Ming.
Alisema baadhi ya makampuni yaliyofika
yana ujuzi mkubwa katika maswala ya gesi asilia na mafuta.
Aliongeza kusema kuwa maeneo mengine
ambayo wanapenda kuwekeza ni pamoja na sekta ya kilimo, mawasiliano, habari na
teknolojia (TEHAMA) na mwaswala ya mipango miji.
Kampuni zilizokuja ni pamoja na Pavilion
Energy, Temasek Holdings, na Singapore Cooperation Enterprise (SCE).
Mwisho
No comments:
Post a Comment