Tuesday, December 17, 2013

Mzumbe Mbeya kampasi yadhamiria makubwa

Na Mwandishi wetu, Mbeya
Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Mbeya umesema umedhamiria kuendelea kuongeza idadi ya wanafunzi mwaka hadi mwaka ili kutekeleza sera ya serikali ya kupanua elimu ya juu na hatimae kuchangia kufikia malengo ya mileniamu.
Akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni baada ya mahafali ya 12 ya chuo hicho jijini Mbeya, Mkuu wa Chuo hicho, Kampasi ya Mbeya, Prof. Ernest Kihange alisema kuwa kampasi hiyo kama sehemu ya Chuo Kikuu Mzumbe imedhamiria kuimarisha majukumu yake ya kufundisha, kufanya tafiti, kutoa ushauri na kutoa huduma kwa jamii ili kuchangia maendeleo katika nchi.
Alisema elimu bora ndio msingi wa maendeleo endelevu na kwamba kampasi hiyo itaendelea kutoa wahitimu bora watakaoweza kupambana na changamoto mara wamalizapo masomo.
“Ni elimu itakayowezesha nchi kufikia malengo mbalimbali ya maendeleo, na sisi tumejidhatiti kutoa iliyo bora,” alisema.
Prof. Kihange alieleza kuwa pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi, watajitahidi pia kutoa elimu bora kwa wanafunzi huku akisisitiza kuwa kufanikiwa kwa wahitimu hao kunategemea kwa kuwango kikubwa wanatumiaje elimu waliyopata baada ya kuhitimu.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Prof. Josephat Itika alisema chuo hicho kitaendelea kuimarisha mitaala na programu mbalimbali ili kuwapa wanafunzi nyenzo zinazohitajika.
Kuhusiana na changamoto za ajira, Prof. Itika alisema chuo hicho kinawaandaa wanafunzi wakiwa bado chuoni ili wajue hali halisi na jinsi ya kukabiliana na mazingira mara wamalizapo masomo.
“Tunapitia mitaala yetu kila baada ya miaka mitatu kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa elimu tunayotoa inaendana na mazingira ya sasa,” alisema.
Awali, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Joseph Kuzilwa alisema kuwa vijana wahitimu hasa toka chuo hicho wanatakiwa kuonyesha kuwa wanaweza kazi kwa kuwa elimu waliyopata ni bora na iliwatayarisha kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Alifafanuwa kuwa pamoja na changamoto za ajira zilizopo nchini, bado nafasi zipo ila kinachotakiwa kwa vijana ni kujiamini na kutumia vizuri elimu waliyopata kwa faida yao nay a nchi.
Jumla ya wahitimu 567 walitunukiwa shahada mwaka huu katika kampasi hiyo kulinganisha na 314 mwaka jana katika programu za astashahada, 235; stashahada, 121; shahada ya kwanza, 173 na shahada ya uzamili, 38.
Kampasi ya Mbeya imeendelea kukua kwa idadi ya wanachuo ambayo imeongezeka kutoka 405 mwaka 2006 hadi kufikia 2241 mwaka huu, hii ikiwa ni ongezeko la takribani asilimia 453.
Kampasi hiyo ilianza mwaka 2006 na kwa kipindi cha miaka sita ya awali ilikuwa inategemea kuendeshwa kutoka makao makuu kwa bajeti ya kawaida.
Baada ya kugatua madaraka na kufuatia ongezeko la udahili la wanachuo, kampasi hiyo sasa inajiendesha yenyewe.
Mwisho.


No comments: