Monday, December 23, 2013

Pinda ataka watafiti wa ndani watumiwe zaidi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa Changamoto kwa taasisi mbalimbali hasa za serikali nchini kuwaamini na kuwatumia watafiti wa ndani badala ya kukimbilia kutumia wale wa nje ambao amesema mara nyingi huwa na gharama kubwa.
Waziri Mkuu alisema hayo wakati alipokuwa akizindua rasmi Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam na pamoja na jengo la ghorofa tano la kampasi hiyo juzi jioni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo baada ya uzinduzi huo, Bw. Pinda alisema kuna tabia imejengeka kwa taasisi na idara za serikali kukimbilia watafiti wa nje pale mahitaji yanapojitokeza na kuwaacha wa ndani.
“Huu mtindo haufai...watafiti wetu wa ndani wana uwezo na wanajua mazingira ya nchi yetu vizuri...tuwasadie kwa kuwapa kazi,” alisema, na kuongeza kuwa serikali inaamini kuwa watafiti hao wanaweza kufanya kazi kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
Alisema watafiti hao wakitumika vizuri watakuwana uwezo wa kutoa majibu yanayolingana na mazingira ya nchi na hivyo kupata suluhisho la changamoto mbalimbali za maendeleo.
Akitoa mfano wa Mzumbe alisema chuo hicho kilichodumu kwa takriban miaka 60 sasa kimetoa mchango mkubwa wa wataalam na kujijengea uwezo katika nyanja mbalimbali ambao unaweza kuwa faida kwa nchi kuliko ilivyo sasa kama kitatumiwa vizuri.
“Tumieni uwezo wa chuo hiki katika tafiti zenu,” Bw. Pinda aliwaambia baadhi ya maafisa waandamizi wa serikali walioandamana nae katika hafla hiyo.
Alisisitiza kuwa katika maswala ambayo vyuo kama hicho vina uwezo nayo hakuna sababu ya kutafuta wataalamu kutoka nje ya nchi.
“Tabia ya kuchua watalaamu kutoka nje ya nchi kwa maswala ambayo wataalamu wetu wana uwezo nayo haiingii akilini,” alisema Pinda.
Aidha  alitoa ushauri kwa chuo hicho kuanzisha kozi fupi amabazo zitasaidia kutoa elimu kwa viongozi wakiwemo mawaziri, wabunge, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wilaya na wengine kupata weledi wa uongozi.
“Kuna matatizo mengi yanajitokeza hivi sasa na ukiyaangalia unakuta kuwa baadhi ya mambo yanahitaji tu weledi wa mbinu kidogo za uongozi,” alisema Bw. Pinda.
Alisema Chuo hicho kilipoanzishwa wakati wa ukoloni na baada ya uhuru kilikuwa kinatayarisha watu kuwa viongozi na kwamba pamoja na kuwa sasa masomo hayo yanatolewa katika programu za masomo ya chuo hicho, bado ipo haja ya kuanzisha kozi hizo fupi kwa ajili ya viongozi ambao hawakupata mafunzo hayo.
Alisifu uongozi wa chuo hicho kwa kupanua wigo wa elimu kwa watanzania kwa kuanzisha kampasi za Mbeya na Dar es Salaam na pia kwa kupanua miundombuni na udahili wa wanafunzi.
Alisema uamuzi wa chuo hicho kutaka kuanza kutoa mafunzo katika ngazi ya uzamili kuwezesha wahitimu kusimamia miradi mikubwa katika sekta za madini, gesi na mafuta ni mzuri na wenye manufaa kwa nchi.
“Kinachotakiwa sasa ni kwa chuo hiki kujenga mahusiano na nchi zenye uzoefu katika sekta hizi ili mjue zaidi undani wake na mboreshe kozi mtakazotoa,” alisema.
Alisema pamoja na kwamba uwiano wa wanawake na wanaume katika udahili wa wanafunzi si mbaya, bado juhudi zinatakiwa katika kuongeza idadi ya wanawake.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa alisema chuo chake kimejenga jingo hilo kutokana na mahitaji makubwa ya  watu wanaotaka kusoma katika kampasi ya Dar es Salaam.
“Jengo hili litasaidia kuboresha huduma zetu kwa wanafunzi na pia kurahisisha kazi ya waalimu wetu,” alisema, na kuongeza kuwa sasa chuo kitaokoa zaidi ya shilingi milioni 300 kwa mwaka zilizokuwa zikitumika katika kukodisha kumbi za mihadhara.
Jengo hilo lina maktaba ya kisasa iliyochukua ghorofa mbili za jengo, ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo pamoja na ya Mkuu wa Kampasi, kumbi tatu za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 132 kila mmoja pamoja na ukumbi wa mikutano.
Alisema chuo kina mipango ya kuongeza ujenzi wa miundombinu na rasilimali watu ili kuzidi kupanua wigo wa elimu kwa watanzania katika sehemu mbalimbali nchini katika juhudi za kuunga mkono nia ya serikali ya kupanua fursa za elimu kwa wananchi.
Kampasi ya Dar es Salaam ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na wanachuo 146 na programu mbili za uzamili.
Katika mwaka wa masomo wa 2013/2014, kampasi hiyo ilidahili wanafunzi 1052 ambao kati yao 504 ni wanawake na 548 ni wanaume wanaosoma shahada za uzamili katika programu zaidi ya 10.
Kukua kwa kampasi hiyo kumechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa Chuo Kikuu Mzumbe ambayo idadi yake kwa sasa ni zaidi ya wanachuo 8,000.
Mwisho. 

No comments: