Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru (kulia) akielezea
jambo kwa Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Afrika ya Kusini, Bi.
Elizabeth Thabethe (katikati) na Balozi wa Afrika ya Kusini nchini Tanzania,
Bw. Thanduyise Chiliza (kushoto). Ujumbe
wa maafisa mbalimbali uliitembelea EPZA jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru (kulia) na
Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha nguo cha Tanzania Tooku Garments
Ltd, Bw. Rigobert Massawe (wa pili kulia) wakitoa zawadi kwa Naibu Waziri wa
Biashara na Viwanda wa Afrika ya Kusini, Bi. Elizabeth Thabethe (kushoto) wakati
ujumbe huo ulipotembelea kiwanda hicho kilicho ndani ya eneo la EPZA jana. Wa pili kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini
Afrika ya Kusini, Bi. Radhia Msuya.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya
Tanzania na Afrika ya Kusini unazidi kuimarika baada ya nchi hizo kufikia
makubaliano ya kuunda vikosi kazi katika nchi hizo ili kuimarisha mamlaka za
ukanda maalum za uwekezaji katika nchi hizo.
Hatua hiyo imekuja baada ya ujumbe wa maafisa
toka serikali ya Afrika ya Kusini kutembelea Mamlaka ya Ukanda Maalum ya
Uwekezaji (EPZA) jana jijini Dar es Salaam.
Ujumbe huo ulioongozwa na Naibu Waziri wa nchi
hiyo wa Biashara na Viwanda, Bi. Elizabeth Thabethe ulikutana na viongozi
waandamizi wa EPZA na kupata fursa ya kufahamu kuhusu mamlaka hiyo na jinsi
inavyofanya kazi hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Meru alisema
Afrika ya Kusini ni nchi yenye uchumi mkubwa barani Afrika na kuwa Tanzania ina
mengi ya kujifunza hasa jinsi mamlaka ya uwekezaji katika maeneo maalum ya nchi
hiyo inavyofanya kazi.
“Tumekubaliana kuunda vikosi kazi katika nchi
zetu ili vifanya kazi ya kuhakikisha kuwa mamlaka zetu zinaimarisha ushirikiano
na kuongeza uwekezaji katika maeneo yetu,” alisema Dkt. Meru.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa Afrika ya Kusini
imekubali kuisaidia Tanzania kutafuta wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika
maeneo ya EPZA hasa katika maeneo ya kuongeza thamani mazao ya kulimo na
madini, kuunganisha vipuri kama magari na maeneo mengine.
Kwa upande wake, Bi. Thabethe alisema kuwa
uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania ni wa muda mrefu na kwamba ni muhimu
ukaimarishwa kwa faida ya watu wa pande zote mbili.
“Ni kupitia biashara na uwekezaji baina ya
mataifa ya Afrika ndipo bara hili litaweza kupiga hatua za kweli za maendeleo,”
alisema.
Alisema Afrika ya Kusini ina mengi ya kujifunza
toka Tanzania na kuwa wako tayari kuimarisha uhusiano huo wa kibiashara na
uwekezaji.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini,
Radhia Msuya alizitaka mamlaka za nchi hizo kufanya kazi kwa karibu ili kufikia
maendeleo endelevu.
“Kuna mengi ya kushirikiana na kufanyia kazi kwa
faida ya watu wetu,” alisema.
Kwa kushirikiana na Afrika ya Kusini, EPZA
itakuwa inaimarisha zaidi mafanikio iliyopata hadi sasa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, pamoja na
kujiwekea malengo ya kuvutia mtaji wa Dola za Marekani 300 milioni kwa mwaka
jana, mamlaka hiyo iliweza kuvuka lengo na kuingiza nchini mtaji wa jumla ya
dola za Marekani 498 milioni nchini, ikiwa ni thamani ya fedha za wawekezaji
walioingia nchini kwa mwaka huo.
Pia mamlaka hiyo ilikuwa imejiwekea lengo la
kuzalisha ajira 5,200 kwa mwaka jana lakini hadi kufikia mwezi Disemba jumla ya
ajira 10,200 zilikuwa zimezalishwa kutokana na uwekezaji mpya uliofanywa
kupitia mamlaka hiyo.
Taarifa zinaonyesha kuwa EPZA ilikuwa imejiwekea
lengo la kuuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 100 2013 lakini lengo
lilivukwa na kufikia dola milioni 105 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana.
Mwisho
No comments:
Post a Comment