Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wakati wafanyabiashara wa Afrika ya Kusini wakionyesha
nia ya kuzidi kuja kuwekeza na kufanya biashara na Tanzania, serikali
imewashauri wafanyabiashara wa ndani kuhakikisha kuwa wanashirikiana nao ili
kusaidia nchi kupiga hatua kiuchumi na maendeleo.
Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda, Bi. Janeth Mbene
alitoa wito huo katika mkutano wa wafanya biashara na wawekezaji wa Afrika
Kusini na Tanzania uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
“Wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika ya Kusini
wameonesha nia kubwa kushirikiana na sisi katika biashara...tutumie fursa hii
vyema,”alisema Bi. Mbene mbele ya waandishi wa habari.
Alisema serikali itakuwa tayari kutimiza wajibu wake
katika kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa bora ili shughuli za
uwekezaji na biashara hapa nchini zinaboreka na kuifanya sekta binafsi kuwa
injini ya uchumi.
“Uchumi wa nchi hiyo ni mkubwa na imepiga hatua kubwa
kiviwanda...itakuwa jambo jema kama tukiimarisha uhusiano na wafanyabiashara
wao,” alisema.
Alisema ushirikiano wa kibiashara unasaidia
kupata maarifa ya biashara, mtaji na kuimarisha biashara, na kuwa fursa hiyo
imekuja katika kipindi mwafaka kwa taifa hili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda
Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru alisema wafanyabiashara
na wawekezaji toka nchi hiyo wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya
ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya Kilimo na madini.
“Wameonyesha nia ya ujenzi wa miundombinu ya barabara,
reli, na bandari,” alisema na kuongeza kuwa pia wameonyesha nia ya
kujenga miundombinu katika maeneo maalumu ya ukanda wa mamlaka yake.
Alisema tayari mamlaka iliwaonyesha maeneo hayo
maalumu ya uwekezaji ambayo yapo katika maeneo mbalimbali nchini na ambayo bado
hayajawekwa miundombinu.
“Kwa bahati nzuri nao wana mfumo kama huu kwetu,”
alisema huku akiongeza kuwa ujio wao uliwawezesha kuona fursa zilizopo na
vivutio vinavyotolewa na mamlaka hiyo na kuwa matarajio ni makubwa kuwa wengi
watakuja kwa ajili ya biashara.
Aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania kuutumia mfumo
wa ushirikiano wa sekta umma na binafsi (PPP) kuwekeza katika miradi mbalimbali
ambayo wanaona wanaweza kufanya hivyo.
Alisema kwa sasa miradi mikubwa inayopewa kipaumbele
katika utaratibu huo wa PPP ni ya ujenzi wa miundombinu.
Alisema hatua hiyo ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara
kwa vile tayari sheria na kanuni za kusaidia kutekelezaji miradi ya namna hiyo
ipo na kuwa kazi imebaki kwa sekta binafsi kufanya kwa vitendo.
Ujumbe wa watu 50 wakiwemo maafisa wa serikali na
wafanyabiashara wa makampuni makubwa 20 ya Afrika kusini walikuwa nchini na
kukutana na wenzao wa Tanzania.
Mwisho
No comments:
Post a Comment