Thursday, January 30, 2014

FSDT yahamasisha wadau wa fedha, wabunifu kushiriki shindano kusaidia wajasiriamali

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Bw. Sosthenes Kewe akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongelea awamu ya tatu ya shindano la mfuko wa ubunifu wa bidhaa za kifedha unaolenga kusaidia wajasiriamali.  Wengine ni washindi waliopita wa shindano hilo; Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Go Finance Limited, Bw. Geoffrey Ndosi (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Problem Solved Limited, Bw. Eric Mutta.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wadau wa sekta ya fedha na wabunifu nchini wametakiwa kuchangamkia awamu ya tatu ya shindano la mfuko wa ubunifu wa bidhaa za kifedha unaolenga kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati.
Shindano hilo linaendeshwa na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) ambao ulianzishwa mwaka 2004 kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha Tanzania hasa kuwezesha watu wengi zaidi na biashara kuweza kufikia huduma za kifedha.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa FSDT, Bw. Sosthenes Kewe alisema shindano hilo lililofunguliwa mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka jana linalenga kuvutia mawazo ya aina ya miradi na ubunifu utakaosaidia kuja na bidhaa na huduma mpya kusaidia wajasiriamali hapa nchini.    
“Hakuna mabadiliko yanayoweza kutokea kama mambo yatafanyika vile vile katika mazingira yanayobadilika kwa kasi,” alisema.
Alisema huu ni wakati wa kwa wadau wa sekta ya fedha na wabunifu kuja na mambo mapya ambayo yatasaidia kuendeleza sekta ya wajasiriamali hapa nchini.
Alisema ingawa umuhimu wa sekta ya wajasiriamali katika kujenga uchumi, kukuza ajira na kuondoa umaskini unajulikana; bado sekta hiyo ina changamoto kubwa kufikia huduma za kifedha.
“Pamoja na umuhimu wao, bado changamoto ya huduma za fedha kwa wajasiriamali hapa nchini ni kubwa sana,” alisema Bw. Kewe.

Kwa mara ya kwanza shindano hilo lilianza mwezi Juni 2011 ambapo katika awamu hiyo kampuni 19 ziliomba; wakati kampuni 13 zilijitokeza katika awamu ya pili ya shindano hilo.

Mshindi wa kwanza, Go Finance Limited, alishinda ruzuku ya dola za kimarekani 153,000 Januari 2012 na ametengeneza mfumo wa kiteknolojia ambao umerahisisha kutoa mikopo kwa wajasiriamali bila kukumbana na masharti magumu katika uendeshaji wa biashara zao.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Go Finance Limited, Bw. Geoffrey Ndosi alisema ruzuku hiyo imesaidia kampuni yao kukua kibiashara, kuongeza ajira pamoja na kusaidia wajasiriamali.

“Ninawahamasisha wadau wa sekta hii kuchangamkia fursa ya shindano hili ili waweze kuleta mabadiliko yanayotakiwa,” alisema.

Mshindi mwingine wa awamu ya pili ya shindano hilo ambaye ni kampuni ya Problem Solved Limited, alijishindia ruzuku ya dola za kimarekani laki 328 (Tshs 525 milioni) baada ya kuelezea jinsi anavyoweza kutengeneza mfumo wa kompyuta utakaosaidia wajasiriamali kutunza kumbukumbu za hesabu zao za biashara kwa urahisi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Problem Solved Limited, Bw. Eric Mutta alisema ruzuku aliyopata itasaidia kuleta tofauti kubwa kwa wajasiriamali hapa nchini na hivyo kuendeleza uchumi wa nchi.

Ruzuku hiyo ya FSDT inatolewa baada ya kushindanisha watu waliyoomba kuanzia dola 100,000 na dola 500,000 kulingana na aina ya mradi.  FSDT hutoa asilimia 50 ya fedha zilizoombwa kusaidia gharama za kuanzisha bidhaa au huduma zikilenga kuinua wajasiriamali.

Mwisho


No comments: