Sunday, February 2, 2014

Sekta binafsi, wadau wa maendeleo watakiwa kushiriki mkutano kuhusu mitaji ya ubia



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Changamoto imetolewa kwa wadau wa sekta binafsi na maendeleo Tanzania kuhudhuria mkutano unaohusu mpango wa mitaji ya ubia (Venture Capital and Private Equity Investment Financing Industry in Tanzania) unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Alhamis wiki hii.
Mkutano huo wa siku moja unaotarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu unatarajia kuongelea jinsi sekta binafsi inavyoweza kufaidika na mitaji ya ubia.  
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta Binafsi (TPSF), Bw.Godfrey Simbeye alisema mkutano huo unatarajia kushirikisha wadau mbalimbali na kujadili kuhusu namna mitaji ya ubia inavyoweza kusaidia kuimarisha uwekezaji Tanzania.
Mkutano huo umetayarishwa na TPSF kwa kushirikiana na TMS Consultants Ltd.
“Tutazungumzia namna ya kuutumia mfumo huu kupata mitaji, ujuzi na teknolojia na kuchochea kasi ya maendeleo,” alisema.
Akielezea zaidi alisema mfumo huu wa mitaji ya ubia unatoa fursa kwa wenye mitaji mikubwa kuingiza mitaji yao, ujuzi na teknolojia kwenye miradi au kampuni ambazo zina miradi lakini zinashindwa kufikia malengo.
Alisema muda umefika kwa wafanyabiashara nchini kuingia katika soko la mitaji ya ubia kwa kuwa mitaji hiyo siyo mikopo.
Bw. Simbeye alisema tatizo la kukosa mitaji ni kubwa sana kutokana na masharti magumu katika mifumo ya kibenki hapa nchini kwa maendeleo ya sekta binafsi. 
Alisema Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Taifa ya maendeleo 2025 zinaelekeza kuimarisha uwekezaji kama moja ya kufikia ustawi wa jamii na kuwa mfumo huo wa mitaji ya ubia unauwezo mkubwa wa kufanikisha hilo.
Inatarajiwa kuwa wadau mbalimbali watashiriki mkutano huo ikiwa pamoja na wafanyabiashara, wabia wa maendeleo, serikali, mashirika ya mifuko ya hifadhi ya jamii, soko la mitaji na wengineo.
Akitoa mfano alisema nchi za Afrika ambazo zimenufaika na mitaji ya ubia ni pamoja na Kenya, Nigeria na Afrika Kusini na kusema hakuna sababu kwanini Tanzania isifanikiwe kupitia mpango huo.
“Mfumo huu unatumika hapa nchini, ingawa ni kwa kiwango kidogo, sasa tunaona kuwa wakati wa kufaidika na fursa hizi kwa kiwango kikubwa ni sasa,” alisema.
Mkutano wa wiki hii unaweka msingi wa mkutano wa kimataifa wa maswala ya mitaji ya ubia unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu hapa nchini.
Mada mbalimbali na majadiliano kuhusiana na mitaji ya ubia kutoka kwa wataalamu wa ndani na nje zitawasilishwa katika mkutano huo.
Mwisho

No comments: