Thursday, February 27, 2014

TPA yazihamasisha nchi jirani kuzidi kutumia bandari ya Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imezihamasisha nchi jirani kuzidi kutumia bandari ya Dar es Salaam kwani sasa huduma zake zinaimarika kutokana na maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa.

Kaimu Meneja Mawasiliano wa TPA, Bi. Janeth Luzangi amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa sasa ufanisi wa bandari hiyo unazidi kuwa wa kisasa na haraka.

“Maboresho yanayofanywa na mamlaka yanazaa matunda hivyo nchi jirani zizidi kutumia bandari yetu ili wapate thamani halisi ya pesa yao,” alisema.

Akielezea zaidi alisema bandari ya Dar es Salaam katika mwaka 2012/13 ilihudumia shehena ya jumla ya tani milioni 12.5 ukilinganisha na tani million 10.9 zilizohudumiwa mwaka 2011/12, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.0.

Katika shehena yote iliyohudumiwa mwaka 2012/13, shehena ya nchi zitumiazo bandari  ilikuwa tani million 4, ambayo ni asilimia 32 ya shehena yote.

Jitihada zinazoendelea kufanywa na Mamlaka pamoja, wadau wa bandari  na serikali katika kuimarisha njia kuuza usafirishaji za reli, na barabara na kupunguza vikwazo vya biashara.

“Hii itasaidia sana kuimarisha huduma ya ndani na nchi jirani,” alisema na kuongeza kuwa jitihada za kimasoko zinafanywa na Mamlaka na wadau wengine kuvutia wateja ikiwa ni pamoja na kuboresha utendaji kazi wa bandari.

Akitoa takwimu zaidi, Bi. Luzangi alisema shehena yote ya mizigo ya nchi 6 zitumiazo bandari ya Dar es salaam, (yaani Zambia, D R Congo, Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda) imeongezeka kutoka tani millioni 3.55 mwaka 2011/12 hadi kufikia tani millioni 4.05 mwaka 2102/13, hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.2.

“Ongezeko hilo ni kutokana na kuendelea kukua kwa uchumi wa nchi hizo na vile vile mazingira mazuri ya biashara humu nchini Tanzania na uboreshaji wa huduma katika bandari ya Dar es Salaam,” alisema.

Akizungumzia ushindani, alisema bandari ya Dar es Salaam iko katika nafasi nzuri zaidi ya ushindani kulinganisha na bandari nyingine katika eneo hili la Afrika kutokana na eneo zuri kijiografia na kuwa nchi inafanya kila kinachotakiwa ili kufanya vizuri.

Katika miaka ya hivi karibuni pamekuwepo na mikakati mbalimbali inayofanywa na serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, TPA pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa bandari ya Dar es Salaam inatoa huduma bora kwa wateja wa hapa nchini pamoja na wale wan chi jirani.

Kutokana na mikakati hiyo pamekuwepo na ongezeko la shehena, tija katika kuhudumia shehena na meli zinazotumia bandari hiyo, na kupungua kwa msongamano wa meli.

Pia kumekuwepo na punguzo kubwa la mrundikano wa mizigo na kufanikiwa kukomesha vitendo vya upotevu wa mizigo na wizi kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano, kwa upande wa mapato, mwaka 2012/13 wastani wa Tshs bilioni 371.7 zilikusanywa, sawa na ongezeko la asilimia 14.3 ukilinganisha na Tsh. bilioni 325.3 mwaka 2011/12.

Katika mapato hayo, bandari bila ya makusanyo ya TICTS, ilikusanya Tsh.bilioni 324.5 mwaka 2012/13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.9, ikilinganishwa na mapato ya Tsh.bilioni 272.9 mwaka 2011/12.

Kwa mujibu wa afisa huyo, matukio ya uhalifu na wizi yamepungua sana kutoka matukio 21 mwaka 2011 hadi matukio 7 mwaka 2012, na kufikia matukio 3 mwaka 2013.

Alisema hali hiyo imetokana na mikakati mbalimbali inayochukuliwa na mamlaka ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vya kisasa katika udhibiti wa uingiaji bandarini, uboreshaji wa miundombinu, mafunzo kwa askari na dhana ya ulinzi shirikishi kwa wafanyakazi na wateja.


Mwisho

No comments: