Mwandishi wetu, Manyara
Wajumbe wa Baraza la Biashara
la Mkoa wa Manyara wameshauriwa kuchapa kazi kwa bidii na kuongeza ushirikiano miongoni
mwao ili kuzidi kusaidia kujenga mazingira bora ya biashara na uwekezaji mkoani
humo kwa maendeleo ya mkoa na nchi kwa ujumla.
Katibu Mtendaji wa Baraza la
Taifa la Biashara (TNBC), Bw. Raymond Mbilinyi aliwaambia waandishi wa habari mkoani
humo mwishoni mwa wiki kuwa wajumbe hawana budi kuhakikisha wanafanya kazi kwa
ushirikiano zaid ili kukuza shughuli za biashara na uchumi.
“Napongeza baraza hili ambalo
limejumuisha wajumbe kutoka sekta ya umma na binafisi kwa kuonesha mwamko mkubwa
wa kufanya kazi,” alisema.
Alisema biashara na uwekezaji
katika mazingira ya sasa unategemea sana ushirikiano wa sekta ya umma na
binafsi kukaa pamoja na kujadili namna ya kuendeleza biashara na uwekezaji.
Alisema wajumbe wa baraza wanatakiwa kujadili kwa uwazi vikwazo na njia
ya kuyatatua na pale inaposhindikana yapelekwe kupatiwa suluhisho katika ngazi
ya taifa.
Alisema Desemba mwaka 2013
ulifanyika mkutano wa saba wa Baraza la Biashara la Taifa, chini ya Uwenyekiti
wa Rais Jakaya Kikwete na ajenda zilikuwa tatu ikiwemo watanzania kushiriki
katika uchumi, Matokeo Makubwa Sasa na kuboresha mazingira ya biashara.
Alisema ajenda hizo zinatakiwa
kufanyiwa kazi katika ngazi ya mkoa ili kupata ufanisi zaidi.
“Nitafurahi kuona baraza la
mkoa huu mkiendeleza hili kwa nguvu ili kufikia malengo yanayokusudiwa,”aliongeza
kusema Bw. Mbilinyi.
Akifafanua zaidi alisema ngazi
ya mkoa na wilaya zikiweka mazingira bora ya biashara itasaidia wafanyabiashara
kushiriki vema na kuwa hayo yote yanategemea zaidi wajumbe hao wa baraza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Manyara, ambaye pia Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Elaston
Mbwilo alisema sekta ya umma itahakikisha inashirikiana vizuri na sekta binafsi
kupitia baraza hilo.
“Sekta ya umma itafanya kazi
kulingana na jinsi tunavyojadili hapa katika kukuza biashara na uwekezaji,”
alisema Bw. Mbwilo.
Alisema mkutano huo ulikuwa
ni fursa kubwa kwao kuzungumzia maswala yanayolenga kujenga biashara na
uwekezaji wa mkoa wao.
Pia alitoa wito kwa baraza
hilo kuziunganisha sekta ndogo za ufugaji na Kilimo ambazo ndizo shughuli kuu
za mkoa huo lakini zimekuwa hazina mahusiano mazuri.
Aliagiza kufanyika kongamano
ambalo litawaunganisha wafugaji kwa kuwa hawana umoja kama ilivyo kwa wakulima.
Mwisho
No comments:
Post a Comment