Tuesday, February 18, 2014

Wajumbe Baraza la Biashara Mkoa wa Manyara wakutana leo

Na Mwandishi Wetu, Manyara
MKUTANO wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Manyara ambao ulikuwa unasubiriwa kwa muda mrefu tangu kufanyika kwa Kongamano kubwa la Uwekezaja mwaka jana unafanyika leo chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa huo,Bw. Elaston Mbwilo.
Bw. Mbwilo aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kwamba maandalizi yote ya mkutano huo muhimu yamekamilika na moja ya agenda kuu itakuwa matokeo ya kongamano la uwekezaji na utekelezaji wake.
 “Wajumbe wote kutoka sekta za umma na ile binafsi wamethibitisha ushiriki wao hapo kesho (leo) na kila kuhusiana na mkutano wetu kipo safi,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Bw. Mbwilo ambaye ni Mwenyekiti wa baraza la mkoa huo alisema mkutano huo una maana kubwa sana ukizingatia kuwa mwaka jana uliandaa kongamano kubwa la uwekezaji ambalo lilivuta wawekezaji wengi wa ndani na wale wan je hivyo utatoa nafasi kubwa kwa wajumbe kujadili matokeo yake kwa kina.
 “Wajumbe wa baraza watapata fursa ya kupitia utekelezaji wa mambo yote yaliyokubaliwa wakatin wa kongamano ambalo lilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda,” Bw. Mbwilo alisema.
Akifafanua zaidi umuhimu wa mkutano huo,Bw. Mbwilo alisema tangu kuanzishwa kwa baraza hilo la biashara mkoa, sekta za umma na binafsi zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu mkubwa sana na hivyo kuibua fursa mbalimbali za kibiashara.
“Mkoa huu Manyara una utajiri mkubwa sana na sisi kama baraza la mkoa tunatumia mikutano kama huu kujadiliana kwa kina ni namna gani tunaweza kutumia fursa hizi kubadilisha maisha ya watu na kujenga kujenga uchumi imara.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mhandisi Raymond Mbilinyi ambaye anahudhuria mkutano huo, amelisifu baraza la Mkoa wa Manyara kwa kuandaa mkutano na kuiomba mikoa mingine kufanya hivyo.
“Sisi kama TNBC tunaunga mkono na kuhamasisha mabaraza yote ya biashara ya mikoa kufanya mikutano yao mara kwa mara iliwaweze kujadiliana mambo mbalimbali yatakayoweza ondoa vikwazo vya kufanya biashara na baadaye kupiga hatua ya maendeleo,” aliongeza Bw.Mbilinyi.
Aliongeza kuwa mabaraza ya biashara ya mikoa yana mchango mkubwa sana katika mikoa husika kwani yamekuwa nguzo muhimu katika kusaidia kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika kufanya biashara.
 “Kupitia mikutano kama hii ya mabaraza, wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi wanapata fursa za kujadiliana na kujua nini hasa kinachelewesha au kinarudisha nyuma jitihada za biashara kukua na kuongeza vipato na kuwezatafutia suluhisho la kudumu,” alisisitiza Bw. Mbilinyi.
TNBC hutoa nafasi ya pekee ya majadiliano katiki ya sekta za umma na binafsi ambapo Rais   Jakaya Kikwete ndiyo mwenyekiti wa Baraza hilo.

Mwisho.

No comments: