Monday, February 17, 2014

EPZA yawaambia wawekezaji kuchangamkia fursa kanda ya ziwa

Na Mwandishi wetu, Mwanza

Wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania wamehamasishwa kuchangamkia fursa katika maeneo maalum ya uwekezaji yaliyo katika kanda ya ziwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalum ya Uwekezaji (EPZA), Dk. Adelhelm Meru ametoa wito huo alipokuwa akiwasilisha mada inayohusu fursa za uwekezaji katika maeneo maalum ya uwekezaji wakati wa kongamano la uwekezaji lililomalizika hivi karibuni jijini Mbeya.
Alisema tayari jumla ya hekari 3,500 zimeshatengwa katika maeneo ya Usagara na Nyangamango wilaya ya Misungwi, Mwanza pakiwa na mpango wa kuyaendeleza kuwa mji wa biashara wenye viwanda vya kisasa.
Pia jumla ya hekari 1,000 zimeshatengwa katika wilaya ya Kahama katika mkoa wa Shinyanga kwa ajili hiyo.
Akifafanua zaidi alisema jumla ya hekari 1,360 zimetengwa wilayani Bunda, mkoa wa Mara.  Eneo hilo pia linakaribishwa kwa wawekezaji kujenga miundombinu, viwanda na mji wa kisasa wa biashara.
“Tutaendelea kwa kushirikiana na mamlaka za mikoa kutenga maeneo zaidi ya uwekezaji katika mikoa ya Kagera, Simiyu na Geita,” alisema.
Akielezea faida za kuwekeza katika maeneo maalum ya uwekezaji katika kanda ya ziwa alisema uwekezaji katika maeneo hayo unasaidia kukuza teknolojia, kuongeza thamani bidhaa, biashara kati ya nchi na nchi, kuongeza ajira, kuongezeka kwa mapato ya kodi kwa mamlaka za ngazi ya chini miongoni mwa faida nyingine.
Alisema mfumo huu wa uwekezaji ni maarufu sana Asia, Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati na kuwa nchi kama China, India, Malaysia, Thailand, Vietnam, Korea, na Philipines zimeimarisha sana uchumi wake kwa kuwekeza katika maeneo maalum ya uwekezaji.
Akitoa mfano zaidi alisema katika miaka 30 iliyopita nchi ya China imefanya kile kinachoonekana kama ‘miujiza’ kutokana na maendeleo iliyojipatia katika maendeleo ya haraka ya uchumi katika historia ya mwanadamu. 
Akitumia takwimu za Benki ya Dunia, Dk. Meru alisema pato la ndani la nchi hiyo limekuwa kwa zaidi ya wastani wa asilimia 9 na mwaka 2010 iliishinda Japan na kupanda kuwa nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.
“Ingawa wataalamu, watunga sera, wafanya biashara mbalimbali na wasomi wanajiuliza siri ya mafanikio hayo, kitu kimoja kilicho wazi ni kuwa uwekezaji katika maeneo maalumu na viwanda vimekuwa kichocheo kikubwa sana cha maendeleo ya China,” alisema.
Alisema mamlaka ya EPZA imeshatenga maeneo katika mikoa 19 yenye ukubwa wa hekta 500-9,000 kila moja nchini na kuwakaribisha wawekezaji kujenga miundombinu katika maeneo hayo.
Alitaja maeneo ya fursa katika kanda hiyo kuwa pamoja na kujenga viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani mazao ya kilimo, ngozi, madini, samaki, asali, TEHAMA na biashara.
Mamlaka hiyo inazidi kujenga mizizi nchini.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, pamoja na kujiwekea malengo ya kuvutia mtaji wa Dola za Marekani 300 milioni kwa mwaka jana, mamlaka hiyo iliweza kuvuka lengo na kuingiza nchini mtaji wa jumla ya dola za Marekani 498 milioni nchini, ikiwa ni thamani ya fedha za wawekezaji walioingia nchini kwa mwaka huo.
Pia mamlaka hiyo ilikuwa imejiwekea lengo la kuzalisha ajira 5,200 kwa mwaka jana lakini hadi kufikia mwezi Disemba jumla ya ajira 10,200 zilikuwa zimezalishwa kutokana na uwekezaji mpya uliofanywa kupitia mamlaka hiyo.
Taarifa zinaonyesha kuwa EPZA ilikuwa imejiwekea lengo la kuuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 100 mwaka 2013 lakini lengo lilivukwa na kufikia dola milioni 105 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana.
Mwisho 

No comments: