Monday, February 24, 2014

TTCL yaahidi makubwa mradi wa mawasiliano vijijini


Afisa Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Peter Ngota (kulia) pamoja na Afisa Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bw. Peter Ulanga wakitia saini mkataba wa mradi wa kutoa huduma za mawasiliano vijijini wenye thamani ya Tshs 9.8 bilioni jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Waliosimama ni Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Prof. John Nkoma (kushoto), Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa (katikati) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dr. John Mngodo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imeahidi kutekeleza kwa ufanisi na kwa wakati zabuni iliyoshinda ya mradi wa kutoa huduma za mawasiliano vijijini.
Ahadi hiyo imetolewa na Afisa Mkuu wa Masoko na Mauzo wa Kampuni hiyo, Bw. Peter Ngota alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kampuni hiyo kutiliana saini na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
TTCL inatekeleza mradi huo wenye thamani ya Tshs 9.8 bilioni baada ya kushinda zabuni hiyo.
Ushindi huo unamaanisha kuwa baada ya kukamilisha mradi huo, TTCL itakuwa na uwezo wa kutoa huduma za mawasiliano katika kata 33 zenye jumla ya vijiji 202 vyenye jumla ya wakazi zaidi ya 300,000 katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Tutafanya kwa ubora zaidi katika awamu hii kwa maana tuna uzoefu wa kina kwani kwa sasa tunao wataalamu wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha kusimamia miradi ya aina hii,” alisema Bw. Ngota aliyekuwa akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Dkt. Kamugisha Kazaura.
Bw. Ngota alisema kampuni hiyo ni muhimili wa mawasiliano Tanzania kwa zaidi ya miaka hamsini sasa katika kutoa huduma za mawasiliano hivyo hawana shaka yoyote katika kutekeleza mradi huo.
Katika awamu ya kwanza yenye kata 20 kampuni hiyo pamoja na kampuni nyingine za simu hapa nchini ilishinda zabuni yenye thamani ya Tshs 3.4 bilioni ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.
Bw. Ngota aliiomba Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia pamoja na UCSAF na wadau wengine kuendelea kushirikiana katika kuleta mapinduzi ya mawasiliano bora kwa wananchi wengi ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Awali, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa alisema serikali inatambua umuhimu wa watoa huduma za mawasiliano katika kupeleka mawasiliano sehemu zenye mawasiliano hafifu.
“Upelekwaji wa mawasiliano umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi wa kijamii katika maeneo hayo,” alisema.
Alisema ni shauku ya serikali kuona kuwa huduma zote wanazofurahia watu wa mijini kutokana na matumizi ya TEHAMA zinawafikia pia watu wa vijijini ifikapo mwaka 2015.
Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Injinia Peter Ulanga alisema mfuko wake umedhamiria kuona maeneo mengi zaidi vijijini yanafikiwa na huduma za mawasiliano.
“Hii ni kwa mujibu wa dira ya maendeleo ya serikali na mkakati huu utasaidia kufikia maendeleo endelevu hapa nchini,” alisema.
Vijiji husika vya mradi huu viko katika mikoa 16 ambayo ni Arusha, Tabora, Iringa, Kagera, Manyara, Dodoma, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tanga.
Mradi huu ulifadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia UCSAF ambao upo chini ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia umepangwa kumalizika ndani ya kipindi cha miezi nane kuanzia Februari 20 mwaka huu.  TTCL pia itagharamia kiasi cha pesa katika mradi huo.
Kwa kuanzia, huduma zitakazotolewa ni zile za msingi kama huduma za ujumbe mfupi, mtandao wa intanenti kupitia simu za mkononi na za mezani zisizotumia waya.
Mwisho  

No comments: