Monday, February 24, 2014

Maboresho bandari ya Dar es Salaam yaanza kuzaa matunda

Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bi. Janeth Ruzangi akisisitiza jambo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu matunda ya maboresho ya bandari ya Dar es Salaam yanayofanywa na serikali kupitia Mamlaka hiyo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Maboresho yanayofanywa na serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika kuboresha huduma zinazotolewa na bandari ya Dar es Salaam sasa zimeanza kuzaa matunda.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa TPA, Bi. Janeth Ruzangi aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa bandari imeanza kupata mafanikio katika kuwahudumia wateja wake na maeneo mengine kutokana maboresho yanayo endelea kufanywa.

Katika miaka ya hivi karibuni pamekuwepo na mikakati mbalimbali inayofanywa na serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, TPA pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa bandari ya Dar es Salaam inatoa huduma bora kwa wateja wa hapa nchini pamoja na wale wan chi jirani.
“Takwimu zinaonyesha kuwa maboresho haya yanasaidia sana kuimarisha huduma zetu,” alisema Bi. Ruzangi.  
Alitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa ongezeko la shehena, tija katika kuhudumia shehena na meli zinazotumia bandari hiyo, na kupungua kwa msongamano wa meli.

Pia kumekuwepo na punguzo kubwa la mrundikano wa mizigo na kufanikiwa kukomesha vitendo vya upotevu wa mizigo na wizi kwa kiasi kikubwa.
Akitoa mfano alisema idadi ya meli zinazotumia bandari hiyo imeongezeka kutoka 1,236 mwaka 2011/12 hadi kufikia meli 1,301 mwaka 2012/13.
Kwa upande wa shehena mwaka 2012/13 bandari ilihudumia jumla ya tani milioni 12.5 ikilinganishwa na tani milioni 10.9 mwaka 2011/12, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 15.

Alisema mwaka wa 2012/13 bandari ilizihudumia nchi zinazotumia bandari hiyo shehena ya tani milioni nne ambayo ni sawa na asilimia 32 ya shehena yote.
“Katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2013 tulihudumia tani milioni 7.50 ukilinganisha na tani milioni 6.38 zilizohudumiwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2012, ikiwa  sawa na ongezeko la asilimia 17.6,” alisema Bi. Ruzangi.

Mafanikio mengine ni kupungua kwa siku meli kukaa bandarini kutoka siku 6.9 mwaka 2008/09 hadi siku 4.9 mwaka 2013, ambapo Julai  hadi Disemba 2013 zilipungua hadi kufikia siku 5.6 ukilinganisha na siku 5.9 kipindi cha Julai hadi Disemba 2012, ikiwa sawa na punguzo la asilimia 5.1
Aidha alisema maboresho hayo yamesaidia pia kuongeza mapato.
Mwaka 2012/13 wastani wa Tshs bilioni 371.7 zilikusanywa, sawa na ongezeko la asilimia 14.3 ukilinganisha na Tsh. bilioni 325.3 mwaka 2011/12 

Katika mapato hayo, bandari bila ya makusanyo ya TICTS, ilikusanya Tsh.bilioni 324.5 mwaka 2012/13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.9, ikilinganishwa na mapato ya Tsh.bilioni 272.9 mwaka 2011/12.
Kwa mujibu wa meneja huyo, matukio ya uhalifu na wizi yamepungua sana kutoka matukio 21 mwaka 2011 hadi matukio 7 mwaka 2012, na kufikia matukio 3 mwaka 2013.

Alisema hali hiyo imetokana na mikakati mbalimbali inayochukuliwa na mamlaka ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vya kisasa katika udhibiti wa uingiaji bandarini, uboreshaji wa miundombinu, mafunzo kwa askari na dhana ya ulinzi shirikishi kwa wafanyakazi na wateja.
Mwisho .


No comments: