Monday, February 17, 2014

Njia mpya mawasiliano inayounganisha Dar, Unguja na Pemba yazinduliwa

Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Serikali imezindua mradi wa njia mpya ya mawasiliano unaounganisha Dar es Salaam kwa upande mmoja na Unguja na Pemba kwa upande mwingine.

Hatua hii sasa inafanya visiwa hivyo vya Zanzibar kuimarika kimawasiliano hasa katika huduma za sauti na nukushi ambazo kabla zilikuwa si nzuri kutokana na kuelemewa kwa njia ya mawasiliano.

Uzinduzi huo ulifanyika Michakaeni Chakechake hivi karibuni.

Mradi huo wa njia ya mawasiliano umejengwa na Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) ikipata msaada wa fedha na ufundi kutoka serikali ya Japan na NEC Afrika, pia kampuni toka nchi hiyo.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema upanuzi huo wa njia ya mawasiliano ulilenga kuondoa msongamano wa sauti na nukushi za watumiaji wa huduma ya mawasiliano.

Alisema msongamano huo ulisababishwa na matumizi makubwa ya huduma za mawasiliano kwa watumiaji hasa taasisi za fedha, elimu ya juu na wafanyabiashara wakubwa.

“Kwa kutumia njia hii mpya ya mawasiliano wateja wa visiwani watapata huduma iliyotukuka bila usumbufu,” alisema na kuongeza kuwa mradi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Alisema upanuzi huo umegharimu Dola za Kimarekani 1,589,300 na kuwa njia hiyo ni mara mbili ya njia iliyokuwepo hapo awali.  Gharama hiyo pia inahusisha pia maeneo mengine upande wa Tanzania Bara.

“Ni dhahiri kwamba ubora wa huduma zinazotolewa na TTCL kwa visiwa vya Pemba na Unguja sasa umeimarika zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali,”alisema Profesa Mbarawa.

Alifafanua kuwa TTCL inachangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa malengo ya Serikali kupitia sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 inayoelekeza ujenzi wa Jamii Habari.

Afisa Mkuu wa Masoko na Mauzo wa TTCL, Bw. Peter Ngota alisema mradi huo ulisainiwa mwaka 2012 kati ya TTCL  na Kampuni ya NEC Africa kupitia Ubalozi wa Japan nchini na ukaanza kujengwa mwaka 2013.

“Kabla ya mradi huu kulikuwa na njia 32 tu za kupitishia mawasiliano na kusababisha kupungua kwa ufanisi katika harakati za maendeleo na uchumi kupitia TEHAMA,” alisema.

Alisema kwa sasa mradi umeongeza njia ambazo zitasaidia kufanya matumizi mbalimbali ya mawasiliano yakiwemo ya video Conference ambayo haikuwepo hapo mwanzo.

Hafla ya uzinduzi huo pia ilihudhuriwa na Naibu Balozi wa Japan hapa nchini, Bw. Kazuyoshi Matsunaga na maafisa wa NEC Africa.


Mwisho

No comments: