Monday, January 27, 2014

Kigoda ahamasisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa Afrika ya Kusini












Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda (katikati) akipokea zawadi kutoka kwa balozi wa Afrika ya Kusini Tanzania, Bw. Thanduyise Chiliza wakati wa mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika ya Kusini uliofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Kushoto ni Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Afrika ya Kusini, Bi. Elizabeth Thabethe.







Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda wa Afrika ya Kusini, Bi. Elizabeth Thabethe wakati wa mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika ya Kusini uliofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wafanyabiashara wa Tanzania wameshauriwa kuchangamkia fursa za biashara nchini Afrika ya Kusini ili kusaidia kuleta uwiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili zenye mahusiano ya karibu kwa muda mrefu.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda aliwaambia waandishi wa habari wakati akifungua mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika kusini kuwa  watanzania wanatakiwa kutumia ipasavyo fursa za kibiashara  zilizo katika nchi hiyo.
“Afrika ya Kusini inauza zaidi nchini kuliko sisi tunavyouza kwao hivyo kuna kila sababu ya wafanyabiashara wetu kuzidi kufanya juhudi na kupunguza tofauti hii,” alisema.
Alisema Tazania bado haijachelewa ila kinachohitajika ni kupanua wigo wa biashara na viwanda na kuyaongezea thamani mazao mbalimbali yanayouzwa nje.
“Nchi ya Afrika Kusini imefungua milango kwa Tanzania na inawahitaji watanzania kupeleka bidhaa nyingi,” alisema Dkt. Kigoda.
Alisema nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda, hivyo kuzidi kushirikiana nayo kibiashara itasaidia kupiga hatua katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
Pia aliwahimiza wafanyabiashara wa nchi hiyo kuwekeza katika miradi ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuongeza uwekezaji kwa faida ya pande zote na nchi zote mbili.
Akifafanua zaidi alisema asilimia 80 hadi 90 ya mazao kama pamba na ngozi huuzwa yakiwa ghafi nje ya nchi hali ambayo inapoteza mapato makubwa, hivyo kuwepo kwa viwanda kutasaidia kutatua changamoto hiyo na hivyo kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa nchi hiyo wa Biashara na Viwanda, Bi. Elizabeth Thabethe alisema nchi yake ipo tayari kuimarisha biashara na Tanzania ili kuzidi kukuza uchumi wa nchi hizi mbili.
“Nimefurahi kuona Tanzania ina kampuni 120 za wafanyabiashara kutoka nchi yangu na wameweza kutoa ajira 2,000...hili linabidi kuimarishwa,” alisema.
Alisema ujumbe wa fanyabiashara alioambatana nao ulikuja kuangalia fursa zilizopo na wanapenda kufanya biashara na Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo za ujenzi wa miundombinu na nishati ya umeme.
Akifafanua zaidi alisema Tanzania inaweza kunufaika zaidi kibiashara hasa katika miradi ya ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP) hasa katika miradi ya kuzalisha nishati.
Alisema kupitia miradi hiyo rasilimali kama makaa ya mawe inayopatikana kwa wingi, inaweza kutumiwa kuzalisha umeme hapa nchini na kuondoa tatizo la nishati ya umeme.
Alisema Tanzania inaweza kupata teknolojia na ujuzi kupitia wataalamu kutoka nchini kwake kupitia ushirikiano wa kibiashara kati ya sekta hizo mbili.
Mkutano huo uliratibiwa na Mamlaka ya Ukanda Maalum ya Uwekezaji (EPZA)  na Wizara ya Biashara na Viwanda na kuwawezesha wafanyabiashara wan chi hizo kukutana na kujadili maswala ya kibiashara.
Mwisho

No comments: