Thursday, December 5, 2013

Waziri Mkuu Pinda kunogesha mahafali Mzumbe leo

Na Mwandishi wetu, Morogoro
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mmoja wa wageni watakaohudhuria mahafali ya 12 ya Chuo Kikuu Mzumbe leo mjini Morogoro.
Bw. Pinda atahudhuria mahafali hayo kama mzazi wa mhitimu mmoja wapo kati ya jumla ya 1748 watakaohitimu katika sherehe za leo.
Kati ya wahitimu wa leo, wawili watatunukiwa shahada ya juu ya uzamivu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Chuo hicho, wahitimu hao ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Njombe, Bi. Pindi Chana pamoja na Bw. Silvius Mbano ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Mkuu wa Chuo, Jaji Mstaafu Barnabas Samatta atatunuku shahada, vyeti na diploma kwa wahitimu katika mahafali hayo.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chuo hicho, Bi. Rainfrida Ngatunga amesema katika taarifa yake kuwa kati ya wahitimu wote wa kampasi kuu 1748, wanaume ni 943 na wanawake ni 814.
Mbali na shahada mbili za uzamivu, wahitimu wa shahada ya uzamili ni 433, shahada ya kwanza 1096 na cheti 215.
“Kwa mara ya kwanza wahitimu 29 watahudhurishwa kutoka katika kituo cha kufundishia cha Mwanza,” alisema Bi. Ngatunga katika taarifa yake.
Mahafali hayo yalitanguliwa jana na siku ya Masahili (Convocation Day), ambapo chuo kimetenga siku hiyo maalumu kwa ajili ya kutambua mchango wa wanataaluma katika chuo hiyo.
“Ni siku muhimu sana kwa familia nzima ya wanamzumbe,” alisema na kuongeza kuwa Chuo kikuu cha Mzumbe kipo makini kuhakikisha kuwa mchango wa wanataaluma unaheshimiwa kwani mchango wao ni mkubwa sana katika maendeleo ya jamii.
Mwisho.


No comments: