Wednesday, October 30, 2013

Rais Kikwete mgeni rasmi chakula cha hisani kuchangia ujenzi wa vyoo barabara kuu

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Hafla ya chakula cha hisani ya kuchangia fedha kwa ajili ya kujenga vyoo vya umma katika barabara kuu za Tanzania sasa itafanyika mwishoni mwa mwezi ujao, Novemba.
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la Mazingira Mufindi (MUET), Bw. Godifrey Mosha aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa chakula hicho kinalenga kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo hivyo katika barabara kuu tatu ziendazo mikoani.
“Tunatarajia kujenga vyoo hivyo katika barabaraza zetu kuu ziendazo mikoani,” alisema,”alisema Bw. Mosha.
Alisema kwa sasa mazingira ya abiria kupata falagha ya kujisaidia barabarani siyo nzuri kwani watu huchimba dawa porini jambo ambalo siyo nzuri kiusalama na husabisha uharibifu wa mazingira.
Barabara zitakazo jengewa vyoo hivyo ni pamoja na Dar es Salaam-Songea;  Mwanza-Dar es Salaam; na Mtwara-Dar es Salaam ambapo awamu ya kwanza itaanza na barabra ya Songea kwenda Dar es Salaam ikiwa na vituo vitano.
Alisema michoro yake imekamilika na inaonyesha umbali wa choo kimoja kwenda kingine na kila choo kitakuwa na matundu hamsini, wanawake 25 na wanaume 25 na cha walemavu na pia sehemu za kuvutia sigara na kutupa takataka.
Awali, chakula hicho cha hisani kilikuwa kifanyike kesho, Alhamis.  Hafla hiyo imesogezwa mbele ili kuleta ufanisi zaidi.
Alitoa wito kwa wadau wote wa mazingira wakiwemo wasafirishaji na watu mbalimbalimbali wazidi kuchangia ili kuzidi kukamilisha shughuli hiyo muhimu kwa maendeleo.
“Vituo hivi vina maana sana kwa abiria na kwa wananchi wa vijiji vya karibu,” alisema na kuongeza kuwa ajira zitazalishwa na kufanya biashara kujiongezea vipato vyao kuendesha maisha yao.
Aliongeza kusema kuwa maendeleo yanakuja kwa wananchi kuwa wabunifu na kushirikiana katika maswala mbalimbali ya kijamii.
Alisisitiza kwamba mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere aliliandaa taifa vizuri na kuliacha likiwa na hali nzuri, hivyo ni vyema sasa kufanya kila liwezekanalo kuzidi kuliendeleza.
Chakula hicho cha hisani kitaandaliwa na MUET kwa kushirikiana na wadu mbalimbali.
Wachangiaji watapatiwa vyeti vya kutambuliwa.
Mwisho.


No comments: