Rais
Jakaya Kikwete akimsalimia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde
la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja wakati akiwasili kuzindua Kambi ya
Vijana ya Kilimo na Maarifa Mkongo wilayani Rufiji hivi karibuni. Wa tatu
kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Profesa Lucian Msambichaka na Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bw. Yamungu Kayandabila
(kwanza kushoto).
Na
Mwandishi wetu, Pwani
Rais
Jakaya Kikwete amesema kambi ya vijana ya kilimo na Maarifa Mkongo iliyopo
wilayani Rufiji mkoani Pwani iwe moja ya mifano hai ya kuondoa umaskini na
kuwakomboa wananchi kivipato.
Rais
Kikwete ametoa changamoto hiyo alipokuwa akifungua rasmi kambi hyo iliyobuniwa
na Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) hivi karibuni wilayani Rufiji.
“Umasikini
wa watu wetu utaondoka kupitia jitihada kama hizi zenye dhamira ya kuwakomboa
kivipato,” alisema na kuongeza kuwa vijana hao wakitumia ujuzi waliopata kwa
vitendo watabadilika kimaisha na watakuwa mfano kwa jamii yote.
Alisema
kambi hiyo ni nzuri kwa vijana na haina budi kutoa mafunzo ya kilimo ambayo
yatawawezesha kwenda kujiajiri na siyo kusubiri ajira ili wakaeneze ujuzi huo
katika maeneo wanayotoka.
Kambi ya
vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo ni moja ya njia za utekelezaji wa azma ya
serikali ya kuleta mapinduzi ya kijani Kupitia mpango wa Kilimo Kwanza.
Kambi
hiyo imeanza na vijana 50, kati ya hao wavulana wakiwa 36 na wasichana 14.
Rais
alisisitiza kwamba vijana hao watakapomaliza mafunzo yao wawezeshwe ili
watakaporudi katika vijiji vyao wakatumie ujuzi walioupata kwa vitendo kupata
fedha.
“Hawa
wakitoka hapa wasiachwe tu, mkiwaacha muda mfupi mtawakuta wanacheza pool…hivyo
ufanyike utaratibu maalumu wa kuwawezesha kwa usimamizi maalumu ili
mashamba yao yakawe kivutio kwa watu wengine kupenda kilimo,” alisema.
Akitoa
mfano alisema mazao nyanya, tikitimaji na matango ya shamba darasa ya kambi
hiyo yana soko kubwa, hivyo watakapomaliza mafunzo hayo wakatumie ujuzi huo
kulima mazao hayo ili kufanikiwa.
Pia
aliitaka RUBADA na Wizara ya Kilimo na Ushirika kuhakikisha wanatafuta aina
bora ya mbegu inayozaa mazao mengi ili vijana hao wakafurahie kazi hiyo na
kuwavutia wenzao na jamii nzima.
Akiongea
wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa RUBADA, Bw. Aloyce Masanja
alisema kambo hiyo pia ni utekelezaji wa mpango wa kukuza kilimo katika ukanda
wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) ambao unalenga kuleta mapinduzi ya haraka ya
kilimo kikanda unaojumuisha jitihada na nguvu za pamoja za wadau mbalimbali.
RUBADA
inatekeleza mpango huu kwa mtindo wa “Hub and Spoke” ambapo mwekezaji mkubwa wa
ndani au wa nje anakuwa “Hub” na wakulima wadogo wanakuwa “Spoke” wote kwa
pamoja wakisukuma gurudumu la maendeleo.
Akifafanua
zaidi alisema mtindo huu unahusu kuanzisha kambi za vijana kwa kila eneo lenye
mwekezaji mkubwa katika bonde zima la mto Rufiji linaloanzia mkoa wa Pwani,
Morogoro, Iringa, Mbeya, sehemu ya Dodoma, Singida, Ruvuma na Lindi.
Bw.
Masanja alisema kufuatana na mkakati sa SAGCOT uliobainisha kongani sita za
Rufiji, Kilombero, Ihemi, Mbarali, Ludewa na Sumbawanga; RUBADA, imeandaa
mpango kabambe wa utekelezaji ambao utashirikisha vijana katika kila kongani.
“Kwa
mwaka huu wa fedha, tunategemea kuwa na vituo vitano vya vijana katika kilimo
na maarifa na kila kituo kitakuwa na vijana wasiopungua 300 ambao watapata
mafunzo katika kipindi cha mwaka mmoja,” alisema.
Vituo
hivyo vya vijana vitakuwa na majukumu ya kutoa mafunzo kuhusiana na utekelezaji
wa kilimo bora chenye tija; kuongeza thamani mazao; matumizi ya vifaa vya
kisasa; utekelezaji wa kilimo bora bila uharibifu wa mazingira; kuandaa andiko
la mradi ili kuweza kupata mikopo katika taasisi za fedha na uundaji wa vikundi
vya ushirika.
Kwa
mujibu wa Bw. Masanja, mafunzo katika kambi hizo yatajikita katika maeneo makuu
matatu yakihusisha uzalishaji wa mazo ya kilimo kwa wingi na yenye thamani
kubwa hasa mazao ya bustani, mboga mboga na matunda; ufugaji wa kisasa wa
ng’ombe na kuku na ufugaji wa samaki pamoja na ujasiriamali.
“RUBADA
inatarajia kuzalisha vijana 600 kutoka kituo cha Mkongo hadi 2015 ambao
watakuwa na utaalamu na ujuzi wa kilimo chenye tija na ufugaji wa kisasa,”
alisema Mkurugenzi huyo.
Kilimo ni
moja ya sekta zinazolengwa katika mikakati mbalimbali ya serikali katika
mapinduzi ya kiuchumi na kufikia malengo ya Milenia na Dira ya Taifa ya
Maendeleo ya 2025.
Kulingana
na sense ya watu ya 2012, asilimia 60 ya nguvu kazi ya Tanzania ni vijana.
Mwisho
No comments:
Post a Comment