Saturday, October 5, 2013

Tanzania yaongeza juhudi kujenga mazingira bora ya biashara mipakani

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye akizungumza katika warsha ya kutathimini, kuongeza kasi na ubora katika Utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini jana jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani, Bw. Mbarak Abudulwakil (katikati)
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka akizungumza katika warsha ya kutathimini, kuongeza kasi na ubora katika Utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini jana jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imewahakikishia wafanyabiashara kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya biashara za mipakani ili kuvutia uwekezaji kwa ustawi wa jamii na uchumi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa swala hilo ni la muhimu na la msingi sana kama nchi inataka kuzidi kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufikia maendeleo endelevu.
“Katika utaratibu wa soko huria ni wajibu wa serikali kuweka mazingira mazuri ya biashara na kuleta ustawi na ushindani kwa sekta binafsi kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Alisema sekta binafsi inapokuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji inasaidia kukuza uchumi, kuongeza ajira na upatakanaji wa mapato ya serikali.
Alifafanua kwamba mazingira ya biashara na uwekezaji yanapokuwa magumu wanaoteseka ni wananchi wa kawaida kutokana na kukosa ajira na huduma muhimu.
Alisema pamoja na kwamba mazingira yaliyopo bado hayakidhi vigezo vya kimataifa, serikali inashirikiana na sekta binafsi katika kuboresha mazingira hayo.
 Alisema maboresho yaliyofanywa yamesaidia biashara na uwekezaji kufanya vizuri na hatua zaidi zinachukuliwa za kuboresha sera na sheria ili hata uchumi uweze kukua kwa asilimia 10 kwa mwaka.
Alisema azma hiyo ni ya dhati katika kuhakikisha mazingira yanakuwa wezeshi, na kuchochea wananchi kutumia fursa na rasirimali zilizopo kuchangia uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye alisema mpango wa kuimarisha biashara mipakani ukizingatiwa utasaidia sana kuimarisha biashara na uwekezaji.
Mpango huo unawaleta pamoja wataalamu kutoka sekta ya umma na wawakilishi wa sekta binafsi kuchambua, kupanga na kutathmini hatua za kuboresha mazingira ya biashara katika maeneo ya mipaka.
Alisema lengo lake ni kuainisha vikwazo na hatua ambazo wizara na taasisi za serikali zinahitajika kuchukua kwa kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kuboresha mazingira hayo.
Akitoa mfano alisema biashara za mipakani imekuwa na vikwazo vingi ambavyo vinajadiliwa kupata ufumbuzi ili bidhaa kutoka bandari ya Dar es Salaam ziweze kwenda nje ya Tanzania bila vikwazo.
Alisema Wizara ya Mambo ya Ndani imejitahidi kurekebisha mazingira hayo na sasa warsha hii itasaidi sana kupata ufumbuzi zaidi wa biashara za mipakani.
Alisema sekta binafsi, imeunda vikosi kazi vinne ambavyo kazi yake ni kufuatilia utekelezaji wa mpango huo kuanzia kuanzisha na Kufunga Biashara, Biashara za Mipakani, Upatikanaji wa Vibali vya Ujenzi na Kuandikisha Raslimali. 
Alisema tathmini iliyofanyka Machi mwaka 2012 na mshauri elekezi kuhusu utekelezaji wa mpango huo inaonyesha kuwa kati ya hatua 193 zilizotakiwa kuchukuliwa, ni 43 tu ikiwa sawa na asilimia 22 tu zilizotekelezwa kikamilifu.
Alisema taarifa za Benki dunia zinazotolewa kila mwaka zinaonyesha Tanzania bado ipo chini katika kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji ukilinganisha na nchi 185 duniani.
Alisema Rais wa Jakaya Kikwete alianzisha mchakato wa Tanzania kuboresha nafasi yake kimataifa katika wepesi wa kufanya biashara kutoka nafasi ya 120, hadi chini ya 100 ifikapo 2011.
Alisema pia hadi kufikia mwaka huu Tanzania bado haijapiga hatua ya kuridhisha na kwamba bado kuna changamoto zinazohitaji utelekezaji kufikia hatua hiyo.
Washa hiyo ya siku mbili ilishirikisha washiriki toka sekta ya umma na binafsi kufanya tathimini, kuongeza kasi na ubora katika utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Mwisho

No comments: