Thursday, October 10, 2013

Wekezeni katika maeneo maalumu ya EPZA - Dkt. Kigoda

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Adallah Kigoda akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha Kishen Import and Export Limited jana jijini Dar es salaam. Kushoto ni Naibu Waziri wa wizara hiyo Bw. Gregory Teo; Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi wa kampuni ya Kishen Import and Export Limited, Bw. Rajen V.Solanki.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Adallah Kigoda (katikati) akisikiliza kwa makini maelezo ya namna ya utengezaji wa pikipiki kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Kishen Import and Export Limited, Bw. Rajen V.Solanki (kushoto) wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) Dkt. Adelhelm Meru.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili kuzidi kuvutia wawekezaji zaidi ili kuifanya nchi kuingia katika uchumi wa viwanda.
Waziri Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda alisema hayo wakati akizidua Kiwanda cha Kishen Import & Export LTD cha jijini Dae es Salaam jana, kuwa mazingira bora ya uwekezaji ni moja ya vigezo muhimu vinavyosaidia nchi kuingia katika uchunmi wa viwanda.
Kiwanda hicho kilichowekeza chini ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) kinatengeneza pikipiki aina ya Toyo za miguu mitatu na miwili.
“Hii ni hatua nzuri na muhimu katika kujenga uchumi wetu,” alisema.
Alisema serikali inajitahidi na imedhamiria kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili taifa liweze kupanua uchumi wake na kutoa ajira kwa watanzania.
Alisema kampuni hiyo ni ya watanzania ambao wamewekeza katika sekta ya viwanda na wanatumia malighafi inayopatikana hapa nchini kwa asilimia 40 na asilimia 60 wapata nje ya nchi.
Alisema watanzania wanatakiwa kuiga mfano huo na kutumia fursa zinazojitokeza na kuwekeza katika maaneo maalumu ya uwekezaji ya EPZA ili washiriki kujenga uchumi wa viwanda.
“Serikali imetengeneza mifumo ya kusaidia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza na kupata mafanikio...wajitokeze na kutumia fursa hizo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru alisema kiwanda hicho kilianzishwa baada ya kupata leseni ya mamlaka yake  na kimeanza kufanya kazi nzuri ya uzalishaji.
“Kiwanda hiki ni moja ya viwanda zaidi ya 70 vilivyo chini ya mamlaka ya EPZA na kinazalisha bidhaa mbalimbali kukidhi mahitaji ya watanzania,” alisema.
Aliongeza kusema viwanda vyote vilivyofanya uwekezaji chini ya EZPA vimewekeza mtaji wa zaidi ya dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 1.15 na kutoa ajira za moja kwa moja  kwa Watanzania 26, 381.
“Haya ni mafanikio makubwa  katika dhana nzima ya kukuza viwanda hapa nchini  na ni matokeo ya azma ya serikali ya kuvutia wawekezaji kujenga uchumi wa kati ifikapo 2025,” alisema.
Alisema EPZA imetenga maeneo ya uwekezaji katika mikoa 20 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na sasa nguvu imeelekezwa zaidi katika maeneo maalumu ya uwekezaji ya Bagamoyo, Mtwara, Kigoma na Dar es Salaam.
Alisema wawekezaji wanatakiwa kuchangamikia maeneo hayo kujenga viwanda ili bidhaa mbalimbali zizalishwe hapa nchini na kupataikana kwa gharama nafuu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw.Rajen V Solank alisema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2012  kutoka kiwanda dada cha Kishen Enterprises Ltd na kinamilikiwa na watanzania kwa asilimia 100.
“Bidhaa zetu ni kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi,” alisema.
Alisema kiwanda hicho kimewekeza dola za kimarekani milioni 3 na kinazalisha pikipiki 300 kwa mwezi na kimeajiri wafanyakazi 270 kati yao 250 ni watanzania.
Alisema pikipiki za miguu mitatu zinapatikana kwa gharama nafuu na zina uwezo wa kubeba zaidi ya tani moja na kutumika kama gari la wagonjwa na shughuli nyingine za uchumi.
Mwisho  


No comments: