Waziri Mkuu Mizengo
Pinda (katikati) akiangalia wakati Naibu Mkurugenzi Mkuu, Ofisi ya Mambo ya
Nje, jimbo la Guandong, China, Bw. Luo Jun (wa tatu kulia) akikaribia
kusalimiana na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu (kushoto)
hivi karibuni. Wa nne kulia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bi. Juliet
Kairuki. Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa
na Waziri Mkuu ulikuwa nchini humo katika ziara ya siku tisa kuimarisha
ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizo.
Na Mwandishi
wetu, China
Waziri Mkuu
Mizengo Pinda amewakikishia wawekezaji wa ndani na nje kuwa tovuti mpya ya
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ni hatua muhimu katika kuimarisha mazingira
mazuri ya uwekezaji nchini.
Waziri Mkuu
amesema hayo mara baada ya uzinduzi wa tovuti hiyo nchini China wakati wa
kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na China katika jiji la Guangzhou
mwishoni mwa wiki.
Ujumbe wa
serikali ya Tanzania ukiongozwa na Bw. Pinda ulikuwa katika ziara ya siku 9
katika nchi ya China kuimarisha uhusiano wa biashara na uwekezaji kati ya nchi
hizo.
Wajumbe toka
kampuni 100 toka China na Tanzania walihudhuria kongamano hilo ambapo mikataba
saba ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ilisainiwa.
“Nawahamasisha
wawekezaji wa ndani na nje kutumia fursa hii muhimu na kufaidika na taarifa
mbalimbali,” alisema Waziri Mkuu, na kuongeza kuwa matumizi ya tovuti hiyo
yatarahisisha kwa kiwango kikubwa utendaji kazi wa wawekezaji.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TIC, Bi. Juliet Kairuki ambaye alikuwa mmoja wa maafisa wa serikali
katika ziara hiyo alisema tovuti hiyo, www.tic.co.tz, itabadilisha
kwa kiwango kikubwa jinsi watanzania, wawekezaji wa ndani na wa nje
wanavyowasiliana na serikali na namna wanavyoshughulikia maswala kama kusajili
kampuni, kujiandikisha katika kulipa kodi na mengine.
“Tovuti hii
inatoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje kupata taarifa zote wanazohitaji
kuhusu kuwekeza nchini Tanzania,” alisema Bi. Kairuki.
Katika juhudi zake za kujenga mazingira bora ya
uwekezaji nchini, TIC inafanya kila linalowezekana kutoa taarifa muafaka na kwa
wakati kwa wawekezaji na wale wanaotarajia kuwekeza.
Akielezea faida za tovuti hiyo, Bi. Kairuki alisema
inatoa taarifa nyingi na kwa uwazi na kuelezea kwa hatua nini kinatakiwa
kufanyika na kwa wakati gani.
“Inaelezea kwa
kina nini kinatakiwa kufanyika na kwa wakati gani,” alisema.
Alisema pia kuwa tovuti hiyo inaelezea gharama rasmi za
serikali zinazotakiwa kulipwa kwa kila hatua ili kuondoa mkanganyiko wowote.
“Taarifa hizo zinapatikana katika lugha zaidi ya 60,
ikijumuisha Kiswahili,” alisema na kuongeza kuwa tovuti hiyo inaelekeza afisa
husika na anuani anayotumia kama itabidi kuwasiliana naye.
Juhudi za TIC kuimarisha utoaji taarifa zake katika mtandao
zilianza Mei 2012 kwa msaada wa kiufundi kutoka shirika la umoja wa mataifa
linaloshughulikia maendeleo na biashara (UNCTAD).
Juhudi hizo zinalenga kuimarisha mazingira ya biashara ya
Tanzania kwa kurahisisha taratibu zake, kuzieleza na kuzitangaza kwa wadau
mbalimbali.
Tovuti hii inaelezea sheria na taratibu zinazotakiwa
kufuatwa kwa uwazi zaidi.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, tovuti inatoa maelezo ya hatua
zinazotakiwa kufuatwa, anayehusika, nyaraka zinazotakiwa kuwasilishwa,
kuchukuliwa, malipo, muda wa kusubiri, sehemu ya malalamiko na sheria
zinazohusika katika kufanya kazi na taasisi za serikali.
“Taratibu
zimerahisishwa kwa kuondolewa hatua za kisheria zisizotakiwa na mahitaji
mengine yasiyokuwa ya lazima,” alisema.
Kupitia tovuti hii,
ni rahisi kwa mjasiriamali kuwasiliana na zaidi ya taasisi za umma 20 na
kuwasiliana na zaidi ya watumishi wa serikali 88 ambao wako tayari kusaidia
katika hatua mbalimbali.
Mwisho
No comments:
Post a Comment