Na Mwandishi
wetu, China
Katika juhudi
za kuimarisha zaidi huduma zake, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimezindua
tovuti yake mpya.
Inatazamiwa
kuwa tovuti hiyo, www.tic.co.tz, itabadilisha kwa kiwango kikubwa
jinsi watanzania, wawekezaji wa ndani na wa nje wanavyowasiliana na serikali na
namna wanavyoshughulikia maswala kama kusajili kampuni, kujiandikisha katika kulipa
kodi na mengine.
Uzinduzi huo
ulitangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Ms. Juliet Kairuki wakati wa
kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na China lililofanyika katika jiji la
Guangzhou nchini China hivi karibuni.
Bi. Kairuki ni
mmoja wa maafisa waandamizi wa serikali walio nchini China kwa ziara ya siku 9
inayokusudia kuimarisha mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya nchi
hizo. Ujumbe huo unaongozwa na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda.
“Tovuti hii
inatoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje kupata taarifa zote wanazohitaji
kuhusu kuwekeza nchini Tanzania,” alisema Bi. Kairuki wakati wa uzinduzi huo.
Katika juhudi zake za kujenga mazingira bora ya
uwekezaji nchini, TIC inafanya kila linalowezekana kutoa taarifa muafaka na kwa
wakati kwa wawekezaji na wale wanaotarajia kuwekeza.
Akielezea faida za tovuti hiyo, Bi. Kairuki alisema
inatoa taarifa nyingi na kwa uwazi na kuelezea kwa hatua nini kinatakiwa
kufanyika na kwa wakati gani.
“Inaelezea kwa
kina nini kinatakiwa kufanyika na kwa wakati gani,” alisema.
Alisema pia kuwa tovuti hiyo inaelezea gharama rasmi za
serikali zinazotakiwa kulipwa kwa kila hatua ili kuondoa mkanganyiko wowote.
“Taarifa hizo zinapatikana katika lugha zaidi ya 60,
ikijumuisha Kiswahili,” alisema na kuongeza kuwa tovuti hiyo inaelekeza afisa
husika na anuani anayotumia kama itabidi kuwasiliana naye.
Juhudi za TIC kuimarisha utoaji taarifa zake katika mtandao
zilianza Mei 2012 kwa msaada wa kiufundi kutoka shirika la umoja wa mataifa
linaloshughulikia maendeleo na biashara (UNCTAD).
Juhudi hizo zinalenga kuimarisha mazingira ya biashara ya
Tanzania kwa kurahisisha taratibu zake, kuzieleza na kuzitangaza kwa wadau
mbalimbali.
Tovuti hii inaelezea sheria na taratibu zinazotakiwa
kufuatwa kwa uwazi zaidi.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, tovuti inatoa maelezo ya hatua
zinazotakiwa kufuatwa, anayehusika, nyaraka zinazotakiwa kuwasilishwa,
kuchukuliwa, malipo, muda wa kusubiri, sehemu ya malalamiko na sheria
zinazohusika katika kufanya kazi na taasisi za serikali.
“Taratibu zimerahisishwa
kwa kuondolewa hatua za kisheria zisizotakiwa na mahitaji mengine yasiyokuwa ya
lazima,” alisema.
Kupitia tovuti hii,
ni rahisi kwa mjasiriamali kuwasiliana na zaidi ya taasisi za umma 20 na
kuwasiliana na zaidi ya watumishi wa serikali 88 ambao wako tayari kusaidia
katika hatua mbalimbali.
Mwisho
No comments:
Post a Comment