Friday, October 11, 2013

Uongozi mpya kampuni ya NICOL wamshangaa Mosha kujihusisha na kazi za Bodi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Menejimenti mpya ya Kampuni ya Uwekezaji ya NICOL imekanusha madai ya Felix Mosha ya kuendelea kujinadi kuwa bado ni mwenyekiti halali wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwa waandishi wa habari jana, Kaimu meneja wa NICOL Kinoni Adam Wamunza, aliwathibitishia wanahisa, na umma kwa  ujumla, kuwa taarifa hiyo ya Bwana Mosha ni hadaa tupu.

Alidxai kuwa lengo la Mosha ni kujisafisha baada ya kesi aliyofungua katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kutupwa nje, na Mahakama kumwamuru Bwana Mosha alipe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo.

Hii ikiwa ni mara ya pili kesi aliyofungua Bwana Mosha inatupwa nje na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Hivi karibuni, Mosha aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye bado ni Mwenyekiti wa NICOL, na atabaki Mwenyekiti mpaka hapo mahakama itakapotoa uamuzi wa kesi (ambayo hakuitaja) aliyofungua Mahakama Kuu.

Katika mkutano huo, Mosha alidai pia kuwa kwa wadhifa wake huo aliwahakikishia wanahisa kuwa amana zao zimekuwa kutoka T.Shs 8.5bilioni mpaka T.Shs 65.0bilioni, kutokana na uwekezaji katika hisa  za NMB.

Hata hivyo, Wamunza amedai katika taarifa yake kuwa Mosha aliongoza NICOL kwa zaidi ya miaka 10 na katika kipindi hicho, ilifika wakati alipuuza kufuata masharti ya usajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), na akawa anaiongoza NICOL kana kwamba ni kampuni yake binafsi.

“Mahesabu ya kampuni hayakuwa yanatayarishwa na kukaguliwa katika muda muafaka. Mahesabu ya NICOL yaliyokaguliwa ni ya mwaka 2008. Aidha, alisimamia uwekezaji katika makampuni ambayo yaliwekwa chini ya ufilisi kipindi kifupi baada ya NICOL kuwekeza katika makampuni hayo,” sehemu ya taarifa hiyo inadai.

Alisema kuwa baada ya kuona Mosha anapuuza mara kwa mara maagizo yao, Taasisi za Udhibiti wa makampuni yaliyosajiliwa katika soko la mitaji; yaani, Msajili wa Makampuni (BRELA), Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA), Soko la Mitaji la Dar es Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA), zililazimika kuingilia kati kwa pamoja na kuwataka wanahisa wa NICOL wachukue hatua stahiki kubadili uongozi wa NICOL uliokuwepo ambao ulionekana kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Kwa kuwa hilo halikufanyika, sehemu ya taarifa hiyo inasema, CMSA ililazimika kuchukua hatua kadhaa za ziada, ikiwa ni pamoja na kuisimamisha Bodi na uongozi wa NICOL na Mosha alikaidi kutekeleza maagizo na maelekezo ya taasisi za udhibiti.

“Baada ya ya miezi tisa kupita, Bwana Mosha alipoanza kuathiriwa na hatua za ziada zilizochukuliwa na CMSA, ndipo alifungua kesi Mahakama Kuu kwa madhumuni ya kupinga maamuzi ya kisheria ya vyombo hivyo, na vilevile kujikinga yeye binafsi,” Wamunza amesema.

Amesema kuwa kutokana na kutoridhishwa na hali iliyokuwepo ya migogoro ambayo ilikuwa inaathiri vibaya utendaji wa NICOL, baadhi ya wanahisa walifungua kesi katika Mahakama ya Biashara, Na. 4 ya 2012, wakaomba mahakama iruhusu mkutano wa wanahisa ufanyike kwa madhumuni ya kubadili uongozi wa NICOL.

Wamunza ameeleza kuwa Mahakama iliridhia ombi la wanahisa na ilitoa Amri kuwa ateuliwe Interim Manager ambaye atachukua uongozi wa NICOL kwa muda kwa madhumuni ya kushughulikia mabadiliko ya kudumu katika uongozi wa NICOL.

“Amri hii ya mahakama mpaka sasa haijatenguliwa, wala hakuna zuio lolote la utekelezaji wake. Mkutano wa dharula wa Wanahisa wa NICOL uliitishwa tarehe 14 Aprili 2012,  kwa mujibu wa Amri hiyo ya Mahakama, ambapo Wanahisa waliazimia, kati ya mengine, kumuondoa Bwana Mosha kutoka uenyekiti wa NICOL, na bodi yake ilivunjwa,” alisema katika taarifa yake.

Katika mkutano wao wanahisa vilevile waliteua Bodi mpya, ambayo sasa ndiyo inatambuliwa kisheria kama alivyohakiki Msajili wa Makampuni (BRELA) kutokana na kumbukumbu za masijala.

“Kwa hiyo ni wazi kabisa kuwa tangu wakati huo Bwana Mosha hatambuliwi kisheria kama Mkurugenzi katika Bodi ya NICOL, au Mwenyekiti wa NICOL,” amesema katika taarifa hiyo.

Aidha, ameeleza kuwa kwa taarifa yake mwenyewe kama ilivyotolewa magazetini, Bwana Mosha amekiri kuwa alifungua kesi katika Mahakama Kuu, na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Suali linakuja, je kama yeye anajinadi ni Mwenyekiti wa NICOL, katika kesi alizofungua anadai kitu gani kama sio kuomba huruma ya Mahakama arudishiwe uenyekiti alionyang’anywa na wanahisa? Kwa maneno mengine, kwa kufungua kesi zote hizo Bwana Mosha anatambua na kukiri kuwa, mpaka hapo mahakama zitakapoamua vinginevyo, yeye sio Mwenyekiti wa NICOL,” Wamunza amesema.

Kuhusu ukuaji wa hisa, ameeleza kuwa asilimia kubwa ya malalamiko yanayopokewa na uongozi mpya wa NICOL kutoka kwa wanahisa yanahusu wanahisa kutopewa taarifa za maendeleo ya kampuni yao kwa muda mrefu;  na kutolipwa kwa gawio, licha ya kuwa waliwekeza ndani ya NICOL miaka mingi iliyopita, tofauti na ilivyo katika makampuni mengine yaliyorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Alisema kuwa hali hii inasababishwa na Mosha kushindwa kutayarisha mahesabu yaliyokaguliwa katika muda muafaka; mahesabu yaliyokaguliwa yaliyopo ni ya mwaka 2008, na yanaonesha kuwa mpaka kufikia mwaka huo, NICOL ilikuwa imelimbikiza hasara ya T.Shs 6.5bilioni.

“Inasikitisha kuona kuwa fedha nyingi za wanahisa zinatumika katika kuendesha kesi zisizo na msingi. Wakati umefika sasa wa kuachana na mambo ya kesi; hivyo basi, kuliko kuendelea kupoteza fedha za wanahisa kwa kuendesha kesi, ingekuwa vizuri kama Mosha angetoa ushirikiano kwa uongozi mpya wa NICOL ili uweze kukamilisha kazi bila vikwazo visivyo na ulazima,” maneja huyo amesema.


Mwisho

No comments: