Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
Mufindi, Bw. William Ntinika (wa kwanza kulia) akizungumza mara baada ya
kuzindua rasmi Chama cha Kuweka na Kukopa cha Kawawa 94 SACCOS limited katika shule
ya Kawawa JKT High School iliyopo Wilayani Mufindi Iringa hivi karibuni. Chama
hicho kimeanzishwa na wanafunzi waliowahi kusoma katika shule hiyo kwa ajili ya
kuwezeshana kivipato, kuenzi shule hiyo na pia kuenzi jina la shule ambalo ni la
Waziri Mkuu Mstafu, Hayati Rashid Kawawa.
Kushoto ni Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Patrick Mavika na katikati ni Mkuu
wa shule hiyo, Meja Hamis Maiga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya Mufindi, Bw. William Ntinika akimkabidhi rasmi cheti Mwenyekiti wa
Chama cha Kuweka na Kukopa cha Kawawa 94 SACCOS limited, Bw. Patrick Mavika (kushoto)
wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa hivi
karibuni.
Na mwandishi wetu, Iringa
Wanafunzi Mkoani Iringa wameshauriwa kuzingatia masomo yao na
kuachana na vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha kukatisha masomo yao na
kuharibu maisha yao ya baadaye.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Kuweka na Kukopa
cha Kawawa 94 SACCOS limited, Bw. Patrick Mavika wakati wa uzinduzi wa chama
hicho wilayani Mufindi mkoani Iringa hivi karibuni.
“Baadhi ya wanafunzi katika mkoa wetu wanashindwa kumaliza masomo
yao kutokana na kujitumbukiza katika vitendo visivyofaa kama utumiaji wa madawa
ya kulevya na vitendo vingine,”alisema.
Chama hicho cha kuweka na kukopa kimeanzishwa na wanafunzi
waliowahi kusoma shule ya Kawawa JKT High School iliyopo Mufindi, Iringa ili
kusaidiana kiuchumi na kuwekeza katika vitegauchumi mbalimbali vitakavyo
waongezea vipato.
“Tumeamua kufanya uzinduzi wa chama chetu katika shule yetu ili
tuweze kuienzi shule hii ambayo tulisomaa na pia kulienzi jina la shule hii la
Waziri Mkuu wa Zamani Hayati Rashid Kawawa,” alisema Bw. Mavika.
Wanafunzi hao wa zamani walichangia tani mbili ya saruji na
mchanga kwa ajili ya kukarabati sakafu ya madarasa yote ambayo yalikuwa katika
hali isiyoridhisha.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Mufindi, Bw. William
Ntinika akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. Christine
Ishengoma alisema wahitimu wa shule mbalimbali mkoani humo wanatakiwa kuiga
mfano huo ili kuendeleza shule walizosoma.
“Wahitumu katika shule zetu wakifanya kama hawa wenzao itasaidia
kuendeleza elimu mkoani hapa na kuendeleza jamii kwa ujumla,” alisisitiza.
Alisema SACCOS hiyo ina masharti nafuu ya kujiunga na kukopa na
inatoa fursa kwa wanafunzi wote waliowahi kusoma katika shule hiyo kujiunga.
Pia alishauri wazazi wenye wanafunzi katika shule hiyo kujiunga na
chama hicho ili kuwawezesha kulipa ada za watoto wao bila usumbufu.
Aidha aliongeza kusema kuwa Mkoa wa Iringa na hasa wilaya ya
Mufindi ni maarufu kwa zao la mbao na sasa kupitia chama hicho wataweza kukopa
fedha na kununua mbao kisha kwenda kuuza katika masoko makubwa.
Mkuu wa shule hiyo, Meja Hamis Maiga alishukuru msaada uliotolewa
na chama hicho cha kuweka na kukopa na kuwa utasaidia shule yake kuwa katika
hali nzuri zaidi.
“Tunashukuru wahitimu hawa na pia sisi tutajiunga ili tuweze
kupata mikopo,” alisema.
Alisema mafanikio ya wahitimu hao na msaada waliotoa kwa shule
hiyo itakuwa ni hamasa kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo shuleni hapo
kujituma kimasomo.
Chama hicho cha Kuweka na Kukopa kimeanza na wanachama 25
wanafunzi waliowahi kusoma katika shule hiyo kuanzia mwaka 1994 ilipoanzishwa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment