Thursday, October 17, 2013

EPZA yakaribisha wawekezaji Bagamoyo

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Litakapokamilika, eneo la kituo cha kibiashara Bagamoyo mkoani Pwani limetajwa kuwa kitovu cha biashara na viwanda vitakavyotumika kuziongezea thamani rasilimali na bidhaa za nchi kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumzia maendeleo ya uendelezaji eneo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru jijini Dar es Salaam jana alisema hatua hiyo itasaidia kuchangia kutatua tatizo sugu la kusafirisha mazao ghafi na hivyo kuikosesha nchi faida ya kutosha.
“Viwanda hivyo vitasaidia kuondokana na tatizo la kusafirisha mazao ghafi nje ya nchi na hivyo kuchangia zaidi pato la taifa na maendeleo kwa ujumla,” alisema.
Alisema eneo hilo litaibadilisha Bagamoyo na kuufanya kuwa mji kisasa wa viwanda na biashara utakaozalisha ajira na kuongeza pato la taifa.
Alisema kuwa viwanda ndio msingi wa maendeleo ya nchi kwa kuwa vinazalisha ajira na kuongeza pato la taifa hivyo kuchangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi kwa haraka.
Alisema kuwa hadi sasa eneo hilo lenye ukubwa wa takribani hekta 9000 tayari limepimwa na kufanyiwa uthamini wa mali zilizopo na ulipaji wa fidia umeanza.
“Tumeshaweza kulipa fidia kwa eneo la takribani hekta 1500 kati ya hizo 9000 na tunatarajia kuendelea kulipa fidia iliyobaki kadiri mapato ya serikali yatakavyokuwa yanapatikana,” alisema.
Alisema kuwa uendelezaji wa eneo hilo umegawanyika katika awamu kubwa mbili ambapo katika awamu ya kwanza yenye hekta 2500 zitaendelezwa na serikali ya China kupitia kampuni ya China Merchants Holdings International Limited.
“Kampuni hiyo itajenga bandari ya kisasa katika eneo la hekta 800 na kuendeleza eneo maalumu la uwekezaji la hekta 1700,” alisema.
Aliendelea kusema kuwa eneo lililobaki linaendelezwa na mamlaka hiyo na kutoa wito kwa wawekezaji ambao wanataka maeneo kwa ajili ya uwekezaji kuwasiliana na mamlaka hiyo ili wapate maeneo hayo kwa shughuli za uwekezaji.
“Kama kuna mwekezaji anataka kujenga kiwanda asisite, aje moja kwa moja katika mamlaka yetu...ili tumpe eneo la kujenga kiwanda azalishe, atoe ajira na kuchangia maendeleo,” alisema.
Aidha alisema kuwa EPZA imeainisha maeneo mbalimbali ya uwekezaji katika mikoa ishirini Tanzania Bara ambayo yamekwishalipiwa fidia na kutoa wito kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kuwasiliana na mamlaka hiyo.


Mwisho

No comments: