Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dkt Adelhelm Meru
akisisitiza jambo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji
nchini (EPZA) imesema ujenzi wa kituo kikubwa cha kibiashara kinachotarajiwa
kujengwa Kurasini jijini Dar es Salaam kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania na
Kampuni kutoka China kitakuwa na manufaa makubwa kiuchumi na ustawi wa jamii.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt.
Adelhelm Meru amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa maendeleo
ya uendelezaji eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha biashara
umefikia hatua nzuri.
“Kituo hiki kinajengwa kwa ushirikiano wa
serikali ya Tanzania kupitia EPZA na Kampuni hiyo ya ubia kutoka jimbo ya Yig
China,”alisema.
Alisema katika kituo hicho kitakuwa na
wafanyabiashara mbalimbali pia viwanda vitajengwa na kitawezesha kutoa
ajira zaidi ya 25,000 kwa watanzania
kitakapokamilika.
Pia kitawezesha bidhaa za mataifa
mbalimbali kupatikana na kupunguza gharama kwa watanzania kwenda nje ya nchi
kutafuta bidhaa hizo.
“Serikali itaongeza wigo wa mapato yake
kutokana na uwekezaji mkubwa utakaofanyika katika kituo hicho,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa ujenzi unatarajia
kuanza baada ya kukamilisha kufanya tathimini na ulipaji fidia makazi ya watu
1012 yaliyopo katika maeneo hayo.
Alifafanua zaidi kuwa ulipaji fidia huo
ulio katika awamu tatu utakapokamilika tu ujenzi wa kituo hicho utaanza mara
moja.
Awamu ya kwanza ya ulipaji fidia imeanza
kutekelezwa ambapo watu 270 tayari wamefanyiwa tathimini na kulipwa na kuongeza
kuwa wamepatiwa miezi miwili kuhama maeneo hayo.
Alisema kwa bahati nzuri baadhi ya wananchi
wameelewa umuhimu wa ujenzi wa kituo hicho kwa ajili ya maendeleo ya nchi na
jamii kwa ujumla.
“Wananchi wanastahili pongezi kwa kukubali
fidia na tayari baadhi yao wameanza kuhama kabla ya muda wa miezi miwili waliyopewa,”
alisema na kusisitiza kuwa wameanza kubomoa nyumba zao kupisha ujenzi wa kituo
hicho.
Alisema nchi nyingi zilizoendelea
zimefanikiwa kwa kutenga maeneo kama hayo ambayo yana viwanda vinavyozalisha
bidhaa mbalimbali.
Alisisitiza wawekezaji kutumia fursa hiyo maana
eneo hilo linaandaliwa kwa ajili ya kituo cha kibiashara ambacho ndani yake
kutajengwa viwanda ili bidhaa zipatikane hapa nchini kwa ghramna nafuu.
Kwa muda mrefu sasa serikali imekuwa katika
juhudi za kupunguza gharama za kufanya biashara hapa nchini na wataalamu
wanasema ujio wa kituo hiki ni moja ya hatua hizo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment