Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bw.
Said Amanzi (katikati) akizungumza na watendaji wa ngazi mbalimbali wa Halmashauri
ya wilaya ya Morogoro wakati wa semina juu ya mpango wa serikali wa Matokeo Makubwa
Sasa na Kilimo Kwanza hivi karibuni Morogoro. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja, na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya hiyo, Bi. Kibena Kingu.
Na
Mwandishi Wetu, Morogoro
Mamlaka
ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) imewataka maafisa ugani katika
halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijijini, kuwa wabunifu katika utendaji wao
wa kazi ili waweze kuongeza thamani ya mazao, pamoja na kutoa elimu stahiki kwa
wananchi wanaowatumikia.
Mkurugenzi
Mkuu wa RUBADA, Bw. Aloyce Masanja alitoa ushauri huo katika halmashauri ya Wilaya
ya Morogoro Mkoani humo wakati wa semina elekezi kwa watendaji wa halmashauri
hiyo juu ya mpango wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa ( BRN) hivi karibuni.
“Ni vyema
maafisa ugani wakaelewa kuwa wao ndio viongozi katika suala la kutoa maelekezo
kwa wananchi wao,” alisema.
Alisema
maafisa ugani waliopo ni wachache kulinganisha na mahitaji yaliyopo katika
vijiji, hivyo kazi kubwa iliyopo ni kujaribu kuwapa elimu ili waendane na mfumo
uliopo na mahitaji ya wakati.
“Tumekuwa
na wagani wachache katika vijiji, japo wanafanya kazi lakini wamekuwa sio mfano
bora kwa wale wanaowatumikia, kutokana na wao wenyewe kutojishughulisha na
kilimo na ndio maana hata wananchi wamekuwa na hamasa ndogo juu ya suala la
kilimo,”alisema Masanja.
Aliongeza
kuwa utamkuta afisa ugani hana hata shamba au mfugo japo mmoja tu jambo
linalosababisha wao wenyewe kutokuwa na mwamko katika sekta ya kilimo na mifugo
katika vijiji wanavyofanyia kazi.
Akizungumzia
suala la upungufu wa maghala ya chakula katika wilaya ya Morogoro vijijini, Bw.
Masanja alisema tatizo hilo linatokana na kuwepo na maghala ya zamani na ambayo
hayana viwango vya kuweza kuhifadhi chakula.
“Katika
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa tunataka kila kijiji kiwe na kilimo cha
umwagiliaji na patajengwa ghala la kisasa kwa ajili ya kuhifadhia chakula,”
alisema.
Alisisitiza
kuwa kwa sasa kuna upotevu mkubwa sana wa chakula hasa mpunga na mahindi
kutokana na kutohifadhiwa katika maeneo maalumu, hivyo kusababisha njaa
zisizokuwa za lazima katika maeneo kadhaa ya wilaya hiyo.
“Watu
hawana ufahamu wa uhifadhi, chakula kimekuwa kikiwekwa chini…ni muhimu swala
hili lirekebishwe,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia
swala la usindikaji katika wilaya hiyo, alisema watu wamekuwa wakiuza mazao
kiholela bila kuyafanyia usindikaji, jambo ambalo limekuwa likiwasababishia
kukosa soko la kueleweka na hivyo kukosa kipato cha kujikimu.
“Chakula
kingi kinauzwa kama kilivyo, badala ya kuuza mchele tunauza mpunga, na badala
ya kuuza unga tunauza mahindi, hili ni tatizo kubwa kwa wakulima,” alisema.
Aliwataka
watendaji kuwaunganisha wananchi wao katika vikundi na kuunda umoja wao, ili
wawe na mashine za kukobolea jambo litakalokuza soko la mazao yao na kuongeza
thamani.
Kwa upnde
wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bw. Saidi Amanzi, alisema serikali ina nia
nzuri ya kuwakomboa wananchi wake kiuchumi, hivyo ni vema wakaunga mkono juhudi
zinazofanywa na serikali yao.
“Sisi
upande wa serikali tunajitahidi kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala la kilimo
chenye tija na kitakachomkomboa mwananchi,” alisema Amanzi.
Aliongeza
kuwa Wilaya ya Morogoro hasa maeneo ya vijijini wamehamasika kwa kiasi kikubwa
na mipango mbalimbali ya serikali ya kukuza kilimo katika maeneo hayo.
Mwisho