Wednesday, May 21, 2014

Dar es Salaam mwenyeji wa mkutano mkubwa wa wanasayansi wiki ijayo

Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini Raslimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Amos Majule (second right) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa anatangaza mkutano mkubwa wa wanasayansi utakaofanyika kuanzia tarehe 27 mwezi huu Dar es Salaam.  Wengine pia wajumbe wa kamati ya maandalizi, Dk. Catherine Masao (kulia), Dk. Stephanie Duvail (pili kushoto) na Bw. Pellage Kauzeni (kushoto).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano kubwa la wanasayansi kutoka bara la Afrika na nje ya bara hilo wiki ijayo kuongelea mabadiliko yanayotokea sasa katika maeneo ya ardhi oevu na makutano ya mito na bahari.

Akitangaza mkutano huo jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi, Prof. Amos Majule alisema kongamano hilo litakalojulikana kama Afrideltas litafanyika kuanzia tarehe 27-30 May 2014.

Prof. Majule ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini Raslimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alitoa wito kwa wadau mbalimbali wanaotaka kuhudhuria mkutano huo wa kihistoria kuhakikisha wanajisajili kwa wakati.

Prof. Majule alieleza kuwa kongamano hilo litahusisha wataalamu wa nje na ndani watakaoangalia na kufahamu zaidi faida zinazopatikana katika maeneo hayo ya ardhioevu na yale maeneo ambayo mto unakutana na bahari.

Alisema mkutano huo pia utapata taarifa mbalimbali za utafiti kutoka nchi nyingine kuhusu maeneo hayo na kubadilishana uzoefu baina ya wataalamu hao.
“Natoa wito kwa wadau wanaopenda kuhudhuria mkutano huu kujisajili mapema,” alisema, na kushauri kutembelea tovuti ya www.kenweb.or.ke au kuwasiliana na taasisi ya IRA kwa taarifa zaidi.

Mtaalamu huyo alisema kuna mabadiliko mengi yanayotokea sasa katika maeneo hayo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za binadamu na hayo yote yanatarajiwa kuangaliwa kwa kina katika kongamano hilo na kuja na maazimio kwa siku zijazo.

Mjumbe mwingine wa kamati ya maandalizi, Dk. Catherine Masao alisema maeneo hayo ni uhimu sana kwa kuwa binadamu wanayategemea kwa maisha yao.

“Maeneo haya yanasaidia na kubeba uhai wa wanyama na mimea,” alisema, na kuongeza kuwa pia maeneo ya ardhioevu yanasaidia katika kurekebisha athari za uchafuzi wa mazingira unaofanywa na binadamu.

Akielezea jinsi mabadiliko ya maeneo ya ardhioevu yanavyoathiri maisha ya watu katika bara la Afrika, mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Dk. Stephanie Duvail alisema ujenzi wa mabwawa katika ukanda wa juu wa mto unaweza kusababisha mabadiliko na katika ardhioevu na kuathiri maisha ya watu.

Akitoa mfano, Bw. Pellage Kauzeni toka Wizara ya Maliasili na Utalii alisema bonde la Kilombero ni moja ya maeneo ya ardhioevu hapa nchini ambayo shughuli za kibinadamu zinapelekea mabadiliko kwa kiwango kikubwa katika eneo hilo.

Katika siku ya tatu ya mkutano huo, inatarajiwa kuwa wanasayansi wataungana na watunga sera na wadau wengine toka serikalini akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu ambae atafunga mkutano ili kujadiliana kuhusu majumuisho na hatua za kuchukua ili kulinda maeneo hayo.


Mwisho.

No comments: