Na Mwandishi Wetu, Tanga
Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kimesema kitaendelea
kuwasaidia wajasiriamali wadogo ikiwa ni njia mojawapo ya kuwajengea uwezo
katika biashara zao ili waweze kukua na kukuza uchumi wao na nchi kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Huduma wa kituo hicho, Mama Nakuala Senzia ameyasema
hayo wakati wa kufunga mafunzo ya siku sita ya wajasiriamali wadogo wapatao 27
wanaojishughulisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka katika mikoa ya Pwani,
Morogoro na Tanga.
“Mafunzo haya ni mwanzo tu wa kuwakuza wafugaji hawa ili
waendelee kuuza maziwa yao kwa ufanisi zaidi,” alisema huku akikitaja kiwanda
cha Tanga Fresh Ltd kama sehemu wafugaji hao wanapoweza kuuza maziwa yao.
Alisisitiza kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana na
serikali ya mkoa wa Tanga na wadau
wengine katika kuhakikisha wanawakuza wajasiriamali wadogo pamoja na kutangaza
shughuli za uwekezaji katika mkoa huo.
“Mkoa wa Tanga una fursa nyingi, hivyo ni jukumu letu
kushirikiana na taasisi nyingine kuwakuza wajasiriamali hawa na kutangaza
uwekezaji katika jiji hili,” alisisitiza.
Aliongeza kua moja ya jukumu kubwa kwa sasa ni kuhakikisha
wajasiriamali wadogo wanakua katika kila kona ya nchi ili kupunguza wimbi la
utegemezi katika jamii na kuhakikisha fursa za uwekezaji zinatangazwa ndani na
nje ya nchi.
“TIC kama moja ya taasisi za serikali tunatambua uwepo wa
wajasiriamali wadogo na tunatambua kuwa wanahitaji kukua kibiashara, hivyo kwa
kufanya hivi tunatimiza azma ya serikali katika kuwainua watu wetu,” aliongeza.
Aidha aliishukuru kampuni ya Tanga Fresh Ltd kwa kusimamia
vema zoezi la uratibu hadi kupatikana wajasiriamali 27 na kuwaingiza katika programu hiyo ya mafunzo
yanayoendeshwa kwa ushirikiano baina ya TIC na Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Maendeleo na Biashara (UNCTAD).
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Tawala wa wilaya ya Tanga,
Bw. Marcelline Patrice, alisema TIC na Tanga Fresh Ltd wamefungua milango ya
mafanikio kwa wajasiriali wa wilaya yake pamoja na mikoa jirani iliyoshiriki
katika mafunzo hayo.
“Muwe makini katika kufanya biashara zenu, naamini sasa
mtakua mmeiva kwa muda mliokaa hapa,” aliwaambia washiriki hao.
Aidha aliwataka wajasiriamali hao kutokuwa waoga katika
suala la kuchukua mikopo katika taasisi za fedha kwani hiyo ndio njia ya kuweza
kuwainua katika biashara zao.
“Wajasiriamali wengi wamekua waoga kuingia katika taasisi
za fedha…waende huko kukopa, ndio mwanzo wa kukua kibiashara,” aliongeza.
Mmoja kati ya wajasiriamali waliopewa mafunzo hayo, Bi.
Beatrice Chanika aliyaelezea mafunzo hayo kuwa ni mkombozi mkubwa katika
shughuli zao za ufugaji.
“TIC waendelee kutusaidia ili tuweze kukua,” alisema
Beatrice.
Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo atakua na uwezo wa
kuweka mahesabu yake katika kumbukumbu sahihi na kuwa atawaelimisha wengine
jinsi ya kutunza maziwa ili yasiweze kuharibika kabla ya kuyapeleka sokoni.
“Elimu niliyopata nitasaidia wenzangu kule Mkinga wajue
jinsi ya kuweka kumbukumbu na kutunza maziwa vizuri,” aliongeza.
Mwisho
No comments:
Post a Comment