Na Mwandishi wetu, Lubumbashi
Serikali ya Tanzania imesema imedhamiria kuhakikisha wafanyabiashara
toka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam
wanapata huduma nzuri kwa faida ya nchi zote mbili.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amesema wakati wa uzinduzi wa
ofisi ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi, DRC
kuwa wizara yake na bandari ya Dar es Salaam watahakikisha kuwa huduma za
bandari zinasogezwa karibu na DRC.
“Nawahimiza wafanyabiashara wa DRC kutumia kwa ufanisi ofisi hii kwa
faida ya jamii nzima ya nchi yao,” alisema.
Waziri alisema kuwa ofisi hizo mpya zitasaidia wafanyabiashara wa DRC
kumaliza matatizo yao Lubumbashi badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.
“Wataweza kufanya malipo ya bandari wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari
ya kusafiri na kiwango kikubwa cha pesa na kuibiwa,” alisema Waziri Mwakyembe.
Alisema tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara hao la
kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa
litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala
wanaokubalika na waaminifu.
Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo
kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.
Waziri Mwakyembe alisafiri kwa barabara tokea Dar es Salaam hadi
Lubumbashi kupitia Zambia kwa barabara zaidi ya kilometa 2000 kuangalia na
kupata taarifa za changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa DRC bandarini
Dar es Salaam njiani wanaposafiri.
Ofisi ya Lubumbashi inalenga kuondokana na changamoto mbalimbali
zinazowakumba wafanyabishara hao zikiwemo ucheleweshaji, wizi, vikwazo
visivyohusiana na kodi na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu.
“Juhudi zinaendelea kuhakikisha kuwa vikwazo na urasimu wote
unaowakabili wafanyabiashara wa Congo unakwisha,” alifafanua Waziri.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter
Serukamba ambaye ni mmoja wa ujumbe wa Tanzania aliyesafiri na Waziri alisema
hatua hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi zote mbili.
Aliishauri TPA kuhakikisha inaweka wafanyakazi wenye moyo na uadilifu
katika ofisi hiyo mpya.
“Naishauri mamlaka hii iweke wafanyakazi wenye moyo na kazi, waadilifu
na wazalendo kwa heshima ya nchi yetu,” alisema.
Makamu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA), Bw. Saidi Sauko amesifu hatua hiyo akisema kuwa itasaidia shirika lao
kuongeza ufanisi wa kazi zao.
Shirika hilo linahusika sana katika kusafirisha mizigo ya DRC kupitia
reli ya TAZARA.
Mizigo ya DRC imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka
tangu mwaka 2004 ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.
Nchi ya DRC ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar
es Salaam. kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua
asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.
Pamoja na maafisa wengine, ujumbe huo ulijumuisha pia maafisa waandamizi
toka TPA, Mamlaka ya Usafiri wa nchi kavu na Majini (SUMATRA), Tanzania
Railways Limited (TRL), TAZARA na wengine.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment