Tuesday, May 13, 2014

Benki ya wanawake yatoa mikopo ya bilioni 20 kwa wajasiliamali

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENKI ya Wanawake Tanzania (TWB) imetoa zaidi shilingi bilioni ishirini (20bn/-) kwa wanawake wajasiriamali na vijana katika jitihada za kuwawezesha kukuza mitaji na kuimarisha biashara zao hapa nchini.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa benki hiyo, Bi. Margreth Chacha, aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa katika kipindi cha chini ya miaka minne tangu benki hiyo ianzishwe maelfu ya wajasiriamali wanawake na vijana wameshanufaika na mikopo ya kuendeleza biashara zao.

“Mikopo yetu kwa wajasiriamali hawa imekuwa kichocheo kikubwa sana katika kupanua wigo wa biashara zao hapa nchini na marejesho ya mikopo hiyo kutoka kwa wajasiliamali na vijana inaridhisha sana na kutia moyo,” Bi. Chacha alisema.

Bi. Chacha alisema benki yake imeona kwamba kuwawezesha wajasiriamali wanawake na vijana ina maana kubwa sana katika kuchangia maendeleo na ukuaji wa shughuli za kijamii na uchumi nchini.

“Ni imani ya benki kuwa wanawake na vijana ni wachangiaji wakubwa katika uchumi wan chi kwani wao idadi yao ni kubwa hivyo endapo watawezeshwa vilivyo basi wanasimama katika nafasi kubwa yab kubadilisha uchumi,” alisema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mwendeshaji huyo, kiasi cha shilingi ya bilioni 17.6 zimetolewa kwa wajasiliamali na vijana kwa mkoa wa Dae es salaam, kiasi  cha bilioni 1.3  kimetolewa kwa wajasiriamali wa  Dodoma na  kiasi cha shilingi milioni 686  kwa wajasiriamali wa Mwanza.

“Wakati sasa tukiwa katika mpango kamambe wa kujitanua kila sehemu hapa nchini, tayari benki yetu imeshatoa mikopo ya kiasi cha shilingi milioni 178 kwa wajasiriamali na vijana mkoani Mbeya na  kiasi cha shilingi milioni 366 kwa wajasirialiamali vijana mkoani Ruvuma.

Bi. Chacha aliongeza kuwa wajasiriamali wanawake na vijana katika mikoa hiyo wamenufaika sana na mikopo ambayo imetolewa na benki na pia biashara zao zinaendelea vizuri sana.

“Wajasiriamali katika mkoa wa Dodoma have walijiunga katika vikundi na mikopo yao waliitumia kununulia mashine za kukamulia mafuta ya arizeti ambapo wale wa mkoaani Mbeya walielekeza katika manunuzi ya mashine za kulimia maarufu kwa ‘power tillers’,” alisema.

Akifafanua zaidi, Bi. Chacha alisema vijana mkoani  Ruvuma wamewezeshwa kupata mitaji pamoja kuwa hawakuwa hata kianzio lakini benki imewawezesha.

“Vijana wapatao 80 wamewezeshwa kukopa pikipiki kwa jina la bodaboda, bajij na magari madogo ya kubebea mizigo na sasa wanazifanyia biashara kubwa mkoani Ruvuma,” alisisitiza Bi. Chacha.

“Tunafanya kila kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa huduma za benki yetu zinakuwepo katika mikoa yote na kuwanufaisha wajasiamali wanawake na vijana nchi nzima,” mkurugenzi mwendeshaji huyo aliongeza.

Tangu kuanzishwa kwake, Benki ya Wanawake nchini imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inawakomboa kimtaji au fedha wajasiriamali wanawake na vijana kuendeleza biashara zao. Pia benki imekuwa ikitoa mafunzo ya ujasiriamali na kutunza kumbukumbu ili waweze kuendesha vizuri biashara zao.

Mwisho.



No comments: