Friday, May 9, 2014

TPA imedhamiria kuongeza ufanisi kwa nchi jirani—Eng. kipande

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) umesema kuwa kufunguliwa kwa ofisi yake ndogo ya mawasiliano nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo ni uthibitisho kuwa kuna nia thabiti kuhakikisha kuwa bandari za Tanzania zinakuwa na ufanisi na ushindani wa hali ya juu katika kuhudumia wateja wake katika eneo hili la Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Madeni Kipande amesema uzinduzi wa ofisi hiyo mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga ni katika moja ya hatua za kuimarisha huduma za bandari ya Dar es Salaam kwa nchi jirani.

“Tuna imani kuwa ofisi hii itasaidia kutatua changamoto zilizopo kwa watumiaji bandari,” alisema.
Inatarajiwa kuwa ofisi hizo mpya zitasaidia wafanyabiashara wa DRC kumaliza matatizo yao Lubumbashi badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.

Pia wataweza kufanya malipo ya bandari wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari ya kusafiri na kiwango kikubwa cha pesa na kuibiwa.

Alisema tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala wanaokubalika na waaminifu.

Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.

Ofisi hiyo ilizinduliwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe siku chache zilizopita.
Akiongelea hatua nyingine kuifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa ya kisasa na shindani, Eng. Kipande alisema kuwa tayari mamlaka hiyo inafanya kazi kwa kutumia mtandao wa kompyuta unaotumia mfumo unaoitwa Harbor View System ambao pamoja na mambo mengine unasaidia kuharakishwa kwa upitiaji wa nyaraka na hivyo kuleta ufanisi.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kuwa TPA imeshakubaliana na kampuni ya Ubelgiji inayoitwa M/S Phaeros ili kuweka na kuanzisha mtambo wa mfumo wa Electronic Single Window System (eSWS) ambao utaunganisha wadau wote wa bandari na kurahisisha kazi kwa kiwango kikubwa.

Mfumo huu utakuwa wa kipekee katika bandari zilizo eneo la Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.
“eSWS itasaidia sana kuongeza ufanisi,” alisema.

Aliwahakikishia wafanyabiashara wa Kongo na nchi nyingine usalama wa mali na maisha yao kutokana na hatua zinazochukuliwa na TPA na wadau wengine.

“Matukio ya wizi yamepungua kwa kiwango kikubwa kutoka matukio 30 mwaka 2011 hadi matatu mwaka 2013,” alisema na kuongeza kuwa katika kipindi chote hicho hakuna kontena hata moja lililoibwa bandarini hapo.

Mizigo ya DRC imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.

Nchi ya DRC ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.  kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.

Mwisho


No comments: