Tuesday, May 13, 2014

TPSF yahamasisha Watanzania kufanya biashara na UN

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta Binafsi (TPSF), Bw.Godfrey Simbeye (katikati) akielezea jambo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Rx Energy, Bw. Francis Kibhisa (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Darworth, Bw. John Kessy wakati wa semina ya kuhamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kutumia fursa zinazotolewa na Umoja wa Mataifa.  Semina hiyo ilitayarishwa na TPSF na ofisi ya UN jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imehamasisha jumuiya ya wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa za biashara katika Umoja wa Mataifa (UN).

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta Binafsi (TPSF), Bw.Godfrey Simbeye katika semina ya kuwahamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kufahamu na kuzitumia fursa za biashara zinazojitokeza katika UN.

Semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni ilitayarishwa na TPSF kwa kushirikiana na kitengo cha manunuzi cha ofisi ya UN.
Bw. Simbeye amesema kuwa semina hiyo ililenga kuwahamasisha wafanyabiashara  ili waweze kuwekeza kimataifa na kutanua wigo wa biashara.

“Tumeleta wafanyabishara wa Tanzania katika semina hii ili kuweza kuangalia ni fursa zipi wanazoweza kuzipata katika zabuni za Umoja wa Mataifa,” alisema Simbeye.

Alisema kwamba Tanzania inashiriki kwa kiwango kidogo sana katika zabuni za UN, kitu ambacho kinawashangaza wadau mbalimbali hasa kutokana na mchango mkubwa wa Tanzania katika kuleta amani kwenye nchi nyingi duniani.

“Hatujafanya semina ya namna hii kwa miaka 9 sasa, kama inavyofanywa na nchi jirani kama Kenya na Uganda…kuna fursa nyingi za biashara na umoja wa mataifa,” alisema Simbeye.

Aliongezea kuwa lengo ni kueleza wafanyabiashara fursa zilizopo, jinsi ya kuzitumia na pia kujua utaratibu unaofanywa na UN katika kupata wazabuni.

Kwa upande wake, Mkuu wa idara ya Manunuzi, UN, Bw. Yavar Khan alisema kuna kila sababu kwa Watanzania kushiriki kwa kiwango kikubwa katika kufanya biashara na umoja huo wa mataifa.

Naye, Afisa Manunuzi Mwandamizi wa Ujumbe wa UN Sudani ya Kusini (UNMISS), Bw. Bruno Maboja alisema kuwa mategemeo yao ni kuona kampuni za Tanzania zinashiriki katika biashara na umoja huo.

Alisema kuwa mwaka 2012 kampuni za kitanzania zilipata mkataba wa dola za Marekani Milioni 7.2, kiwango alichosema ni kidogo.

Mwisho

No comments: