Friday, May 2, 2014

Chiza aipa changamoto Bodi mpya ya RUBADA

Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) baada ya bodi iliyokuwepo kumaliza muda wake mwishoni mwaka jana.
Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza( kulia) akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA),Profesa Lucian Msambichaka (katikati)wakati alipokuwa akizindua bodi hiyo, kushoto ni Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Aloyce Masanja.
 Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam
Wajumbe wa Bodi ya mpya ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) wamepewa changamoto ya kutimiza malengo yote waliyojiwekea katika kipindi chao cha miaka mitatu kwa kuongeza ufanisi zaidi wa mamlaka hiyo .

Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza alitoa changamoto hiyo jijini Dar es Salaamjana wakati akizindua bodi hiyo na kuwataka wajumbe wa bodi kufikia malengo waliyojiwekea na kuifanya RUBADA kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

“Ningependa kuona mnajiwekea malengo yenu na mnatimiza kwa wakati ili mtakapo maliza muda wenu muweze kusema mliiletea mafanikio mamlaka hii,”alisema Mhandisi Chiza.

Alisema wizara yake ina imani kubwa sana bodi hiyo ambayo mwenyekiti wake ni Profesa Lucian Msambichaka ambaye ni miongoni mwa wachumi waliobobea hapa nchini.

Mbali ya Profesa Msambichaka, wajumbe  wengine katika bodi hiyo ni pamoja na Profesa Henry Mahoo, Mhandisi Bashir Mrindoko, Gaspar Luanda, Mhandisi Hosea Mbise, Mhandisi Raphael Dalluti, Dkt. Ben Moshi, Bi.Eline Sikazwe naBi. Nkuvililwa Simkanga.

Aliitaka bodi hiyo kuharakisha zoezi la upatakanaji wa sheria mpya ya mamlaka ili shughuli za uendelezaji bonde hilo zisiweze kukinzana na sheria nyingine.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa pia na Naibu waziri wa wizara hiyo, Bw. Godfrey Zambi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Raphael Daluti.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profsea Lucian Msambichaka alisema atahakikisha maagizo yaliyotolewa na waziri wa kilimo na ushirika yanatekelezwa ili kufikia malengo ya mamlaka.

“Ni lazima tutekeleze majukumu yetu na ninaamini bodi yetu ni nzuri na ina watu muhimu na wenye weledi mkubwa katika kutimiza majukumu,”alisema.

Alisema uongozi wake utahakikisha unachangua baadhi ya miradi na kuifanyia kazi ili bodi itakapomaliza kipindi chake iweze kuonyesha mafanikio yaliyopatikana.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw, Aloyce Masanja alisema uzinduzi wa bodi hiyo mpya anauchukulia kama ni chachu katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Sisi tumejipanga kushirikiana na bodi mpya katika kuhakikisha miradi inayokusudiwa ikiwemo ya Kilimo, na uzalishaji nishati ya umeme inafanikiwa,”alisema.

Alisisitiza kuwa shughuli kuu zinazofanywa na mamlaka ni pamoja na uhamasishaji ,uratibu na udhibiti wa mafuriko na usimamiaji wa shughuli za maendeleo kwenye Bonde la Mto Rufiji.

Alisema bonde hilo linaumihimu mkubwa kwa vile miradi yote ya Mpango wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) inapatika katika bode hilo na miradi yote iliyopo kwenye bonde ni sehemu ya kufikia mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).

Alisema bodi hiyo iliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete Mwezi October mwaka 2013 na sasa imeziduliwa tayari kwa kuanza kufanya kazi rasmi kwa kushirikiana na menejimenti.

Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA ni taasisi ya serikali iliyopewa jukumu la kusimamia na utekelezaji wa shughuli za bonde hiyo.

Mwisho.


No comments: